Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi amewataka wadau wa ajira ikiwemo waajiri, watafuta kazi na wananchi kwa ujumla kujihadhari na wimbi la matapeli ambao wamefikia hatua ya kughushi nyaraka za Serikali.
Amesema ni vizuri wananchi wakatambua kuwa hivi sasa kutokana na kukua kwa teknolojia, njia za mawasiliano zimeongezeka na hivyo kuwafanya baadhi ya watu ambao sio waaminifu na wanaotaka kufanikiwa kwa njia za mkato, kutumia mbinu zisizo sahihi za kuwatapeli baadhi ya wahitimu wa fani mbalimbali katika ngazi tofauti kwa kuwapigia simu kuomba miadi, au fedha ili waweze kuwasaidia kupata kazi na wengine wamekwenda mbali zaidi kiasi cha kughushi barua za ajira.
Ametoa tahadhari hii baada ya ofisi yake kupata malalamiko pamoja na taarifa ya tapeli aliyeamua kwa makusudi kughushi barua ya ajira akijifanya amepata kazi ya Udereva Daraja la II kupitia Sekretarieti ya Ajira baada ya kufanya usaili tarehe 12 Julai, 2018 ikionesha amepangiwa kituo cha kazi Halmashauri ya Wilaya ya Urambo tarehe 14 Novemba, 2020. Sambamba na hilo tapeli huyo amekuwa akipita ofisi mbalimbali zikiwemo taasisi za kidini kuomba achangiwe fedha kwa ajili ya nauli ya kwenda kuripoti kazini mkoani Tabora Wilaya ya Urambo, ilihali akijua ni uongo hajafanya usaili, hajaipata hiyo barua serikalini wala hajapangiwa kituo cha kazi husika.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma anawataka matapeli wote au mtu yeyote yule mwenye nia ya kuendelea na shughuli za kitapeli, kuacha mara moja kwa kuwa mkono wa Serikali ni mrefu na unaweza kumkamata mara moja kama alivyogundulika tapeli huyu ambaye taratibu mbalimbali zinafanyika ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
Aidha, anatoa wito na tahadhari kwa wananchi na wadau mbalimbali kuwa makini na kujihadhari na matapeli hawa ambao wanazunguka maeneo mbalimbali. Serikali inawafuatilia kwa karibu matapeli hao na pia tunawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa Sekretarieti ya Ajira au kwenye vyombo vya dola pale wanapomtilia mashaka mtu ambaye aidha anaahidi ajira kwa njia ya udanganyifu au kuchangisha michango ya nauli kwa kutumia nyaraka zilizoghushiwa.
Ni vyema wadau mbalimbali wa Sekretarieti ya Ajira wakatambua kuwa uendeshaji wa mchakato wa ajira serikalini unazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu na pia hufanywa kwa uwazi kuanzia hatua ya kutoa matangazo kupitia tovuti ya taasisi liwe tangazo la kazi, tangazo la kuitwa kwenye usaili au tangazo la kupangiwa kituo cha kazi.
Pamoja na hayo, mawasiliano hufanyika kwa Mwajiri na Mamlaka nyingine zenye dhamana na masuala ya kiutumishi.
Ni imani yetu wananchi na wadau wa ajira watachukua tahadhari dhidi ya matapeli hao.
Imetolewa na; - Riziki V. Abraham
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.