WAOMBAJI KAZI WENGINE 80 WAPATA AJIRA KUPITIA KANZIDATA

Watanzania wameendelea kunufaika na matunda ya kuanzishwa kwa mifumo mbalimbali kupitia TEHAMA ndani ya Sekretarieti ya Ajira ikiwemo kanzidata (database) ya Waombaji Kazi waliofaulu usaili na kuhifadhiwa humo, ambapo Waombaji kazi wengine themanini (80) wameweza kuitwa kazini kwa mwezi huu nje ya wale waliopangiwa vituo vya kazi mwanzoni mwa mwezi huu ambao walikuwa mia sitini na nane (168) bila ya kurudia kufanya usaili mwingine mara baada ya nafasi wazi za kazi kupatikana ndani ya Utumishi wa Umma.

Hayo, yameelezwa na Naibu Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Lucas Mrumapili alipokuwa akiongea na Watumishi wa Kitengo cha Mawasiliano cha Sekretarieti ya Ajira.

Aidha, amewataka Waombaji Kazi kabla ya kwenda kwenye usaili kuhakikisha wamejiandaa vizuri ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata kazi hata kama wakikosa nafasi ya awali, wasikate tamaa kwani wanaweza kupata kupitia mfumo wa kanzidata ambao umeweza kuwanufaisha Watanzania wengi mpaka sasa.

“Mnaweza kuona kwa mfano mwezi Mei mwaka huu, zaidi ya Waombaji kazi mia mbili arobaini na nane (248) wameweza kunufaika kwa kupangiwa vituo vya kazi kutoka katika Kanzidata” alifafanua Mrumapili.

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (PO-PSRS) - 22 Mei, 2020

Dawati la Msaada na Malalamiko (0735-398259/0784398259 au 0736005511)