SERIKALI INAWATAKA WAOMBAJI WA FURSA ZA AJIRA KUTUMIA NAMBA ZAO ZA NIDA

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inawataka Waombaji Kazi wote wanaotafuta kazi serikalini kuhakikisha wanatumia namba zao halisi walizopewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kuwa imejitokeza tabia ya baadhi ya Waombaji Kazi kutumia namba za NIDA za watu wengine na kujikuta wanaondolewa katika mchakato wa ajira kwa kukosa sifa  kwa mujibu wa tangazo la kazi.

Agizo hili limetolewa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Bw. Xavier Daudi kufuatia changamoto hii kuanza kujitokeza tangu ilipotakiwa Waombaji kazi  serikalini kutakiwa kutumia namba zao za kitambulisho cha NIDA wakati wa kujisajili katika mfumo wa maombi ya kazi unaopatikana kupitia “portal.ajira.go.tz” ambao umeunganishwa katika mifumo mingine ya utambuzi ikiwemo NIDA, NECTA na NACTE na sasa wako katika hatua za kuunganisha pia na mfumo wa kiutumishi (HCMIS),” kwa ajili ya kuhakiki taarifa za waombaji kazi pamoja na matumizi mengine ya Serikali.

Kwa kuwa kumeibuka tabia ya baadhi ya waombaji kazi wasio na kitambulisho ama namba ya kitambulisho cha NIDA, kuamua kutumia namba za watu wengine ili kuweza kujisajili katika mfumo wa maombi ya kazi. Jambo ambalo limechangia baadhi ya Waombaji kazi ambao walikuwa na uwezo wa kupata nafasi ya kuitwa kwenye usaili kuenguliwa katika mchakato kwa kutumia taarifa zisizo za kweli na baadhi yao kuona kama wameonewa kwa kuondolewa kwenye mchakato husika.

“Ni vyema Waombaji wa fursa za Ajira serikalini kutumia namba zao halisi za NIDA badala ya kutumia namba za watu wengine, kwakuwa kufanya hivyo ni kosa la kisheria na inapobainika wahusika huondolewa katika mchakato wa ajira hata kama wana sifa nyingine zote za msingi kwa mujibu wa tangazo la nafasi za kazi” amesisitiza Daudi.

Sekretarieti ya Ajira imebainisha kuwa haitamfumbia macho Mwombaji kazi yeyote atakayekwenda kinyume na Sheria, Kanuni na Taratibu za uendeshaji wa mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma.

Aidha, amewataka wadau mbalimbali hususani waombaji wa fursa za ajira kuingiza wenyewe taarifa zao katika mfumo wa maombi ya kazi badala ya kutoa taarifa zao kwa watu wengine ambao baadhi yao sio waaminifu huweza kuzitumia vibaya, au kuwaingiza kwenye gharama zisizo za lazima.

Ameongeza kuwa ni vyema mwombaji asiyefahamu namna ya kujaza akatumia mwongozo wa namna ya kujaza ulioko kwenye tovuti au akawasiliana na ofisi za Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kupitia simu za kiganjani 0735398259- 0736 005511 - 0784398259 na kupatiwa ufafanuzi ama kufika katika ofisi zao zilizoko Jengo la Utumishi Kivukoni jijini Dar es Salaam.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Sekretarieti ya Ajira

6 Aprili, 2020