Majibu ya hoja na maoni ya wadau kwa mwezi Julai, 2018.

August 2, 2018


Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inaendelea kuwashukuru wadau na wananchi mbalimbali wanaotuandikia maoni pamoja na kuuliza maswali mbalimbali yanayohusu Ajira kwa kipindi cha mwezi Julai,2018.Wale wote waliotuandikia maoni na maswali yao kupitia barua pepe na kurasa zetu za ‘facebook’ na ‘Instagram’ tumeendelea kuwapa majibu ya hoja zao kadri wanavyouliza.

Aidha kwa maswali  yanayofanana na yanayohitaji uelewa wa jumla tumeyaunganisha na kuyatolea majibu kwa faida ya wasomaji wetu wengine ili kuendelea kutoa elimu kuhusu masuala yanayohusu Uendeshaji wa Mchakato wa Ajira Serikalini.

Swali la kwanza.

Je fursa za Walemavu katika mchakato wa Ajira kwa mujibu wa Sheria zinavyozingatiwa?

Jibu.

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inasimamia Sheria, Kanuni na Taratibu katika kutekeleza mchakato wa Ajira Serikalini.

Sheria ya Walemavu Sura 183, Kifungu cha 33 (1) kimeeleza wazi utaratibu unaotakiwa kufuatwa wakati wa kutekeleza mchakato wa Ajira ndani ya Utumishi wa Umma. Sambamba na Sheria hiyo pia Kanuni za Uendeshaji za Sekretarieti ya Ajira za mwaka 2009, Kanuni ya 16 (1) imeainisha wazi wastani anaotakiwa kufikia kila msailiwa ili aweze kuajiriwa kuanzia madaraja ya kuingilia, nafasi za Wanataaluma hadi ngazi ya Watendaji Wakuu.

Kwa kuzingatia msingi huo, Sekretarieti ya Ajira imeweka wazi katika mfumo wake wa uwasilishaji wa maombi ya kazi ikiwataarifu waombaji wa fursa za

Ajira kuainisha katika mfumo na hata kueleza kwenye barua endapo ni mlemavu ili kwanza kuweza kumwandalia mazingira rafiki kulingana na hali yake ili aweze kufanya usaili bila ya matatizo. Sambamba, na hilo pindi inapotokea kuna mlemavu aliyefanya usaili na kufikia wastani unaotakiwa na kufungana na wasailiwa wengine basi msailiwa mwenye ulemavu hupewa kipaumbele cha kupata Ajira.

Swali la pili.

Napenda kufahamu ni namna gani naweza kupata mrejesho baada ya kutuma maombi ya kazi kupitia mfumo wa ajira.

Jibu.

Maboresho yaliyofanyika katika mfumo wa ajira kwa sasa yanampa mrejesho wa aina mbili (2) mwombaji kazi kama ifuatavyo;

Mrejesho wa kwanza ni pale mwombaji anapoomba kazi ambayo hakustahili kuiomba kutokana na sifa zilizopo katika tangazo. Mfumo hautamruhusu kuomba kazi hiyo na utampa sababu ya kutokustahili maombi yake kupokelewa. Mfano, endapo tangazo linamhitaji mwombaji kazi mwenye umri chini ya miaka 45, wale wote ambao umri umezidi hawataruhusiwa kuomba na mfumo utawapa sababu ya kutokubaliwa kuomba kazi hiyo kwa kuwa na umri mkubwa au kama nafasi ya kazi iliyotangazwa inahitaji mtu mwenye elimu ya kiwango cha Astashahada endapo ataomba mtu mwenye kiwango cha elimu tofauti na hicho mfumo pia utampa sababu ya kutokubaliwa.

Pili, mrejesho kupitia akaunti ya mfumo na barua pepe (email). Katika hatua hii mwombaji kazi baada ya kufanikiwa kuomba kazi, atakuwa anapokea mrejesho kulingana na hatua “stage” ya usaili iliyopo. Mathalani, akiomba kazi na kufanikiwa, mfumo utamtumia barua pepe ukimjulisha kuwa maombi yako yamefika na akichaguliwa ‘shortlisted’ mfumo utamjulisha kuwa amechaguliwa kwa hatua nyingine na hata anapofaulu usaili, mfumo una uwezo wa kumjulisha kuwa amefaulu usaili.             

Swali la tatu

Kumekuwa na uelewa tofauti kwa baadhi ya waombaji kazi kuhusu asilimia anazopaswa kuwa nazo mwombaji wa ajira pindi ajazapo taarifa zake katika mfumo, je mnaweza kutoa ufafanuzi katika hili.

Jibu

Tungependa kuwajulisha waombaji fursa za Ajira kuwa, Mfumo wa maombi ya kazi unamhitaji mwombaji aingize taarifa za msingi ambazo hazina tofauti na zile anazoweka katika wasifu wake binafsi (CV). Kinacho ongezeka ni ushahidi wa taarifa zake ambapo vyeti husika pia huingizwa katika mfumo.

Mwombaji kazi kabla hajaanza kuingiza taarifa zake, mfumo humpatia ASILIMIA 0 ya taarifa zake. Anapoanza kuingiza taarifa, mfumo huongeza alama (katika asilimia) za kiwango cha taarifa alizoingiza. Mwombaji anapofikisha kuanzia asilimia 75 ya taarifa zake, mfumo humruhusu kuomba kazi. Sekretarieti ya Ajira tunaamini kuwa taarifa za mwombaji zinapofikia kiwango cha ASILIMIA 75, taarifa zake zinakuwa zinajitosheleza kumfahamu vizuri na hivyo tunampa nafasi ya kuomba nafasi za kazi kupitia mfumo huo unaopatikana kwa anuani ya http://portal.ajira.go.tz

Aidha ni muhimu kutambua kuwa, kuingiza taarifa kwenye mfumo wetu wa maombi ya kazi kwa asilimia zaidi ya 75, hakumfanyi mwombaji kuamini kuwa tayari ameomba kazi, bali atambue kuwa taarifa zake zimejitosheleza na hivyo anayo fursa ya kuomba kazi kupitia mfumo wetu endapo nafasi za kazi zimetangazwa.

Ni muhimu pia kufahamu kuwa mfumo huu umejengwa kwa kuzingatia elimu za wahusika, Kwa maana kuwa hata mwenye Elimu ya kidato cha nne na

astashahada anaweza kuomba kazi kwani aingizapo

Swali la nne.

Je ni kweli kuwa maboresho ya Mfumo yamesaidia kupunguza muda wa mchakato wa ajira?.

Jibu.

Maboresho katika mfumo wa maombi ya kazi umesaidia sana Sekretarieti ya Ajira na Serikali kwa ujumla kupata watumishi wenye sifa kwa wakati. Kwa upande wa Sekretarieti ya Ajira, maboresho haya yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza muda wa mchakato wa Ajira. Kabla ya mfumo huu kuanza, mchakato wa ajira ulichukua siku 72 hadi 90 kuanzia kutangaza nafasi za kazi hadi kupangia kazi waliofaulu, lakini kwa sasa  tunatumia siku 52 na nimatumaini yetu kuwa muda huu utapungua zaidi. Lengo ni kufikia siku 42 ama pungufu ya hapo. Pia, maboresho haya yameufanya mfumo uweze kubaini waombaji kazi ambao hubadilisha taarifa zao ili kuomba kazi. Baada ya maboresho, mfumo unaweza kuweka kumbukumbu ya kila badiliko linalofanywa na mwombaji kupitia akaunti yake na hivyo ni rahisi kuwabaini waombaji kazi wadanganyifu.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.