SEKRETARIETI YA AJIRA YABORESHA MFUMO WA UTUMAJI WA MAOMBI YA KAZI.

March 28, 2018


Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yanazidi kukua kadri  teknolojia inavyobadilika. Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma katika kuboresha utendaji kazi wake ilianzisha mfumo wa kielektroniki unaojulikana kama ‘Recruitment portal’ unaopatikana kwa anuani ya http://portal.ajira.go.tz ambao unamsaidia muombaji kazi kuingiza taarifa zake na hatimaye kutuma maombi ya kazi kupitia mfumo huo.

Baada ya kuanza kutumia mfumo huo mwaka 2014 Sekretarieti ya Ajira imekuwa ikitoa fursa ya kupokea maoni ya wadau mbalimbali hasa watumiaji na kubaini changamoto kadhaa ambazo zimefanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha mfumo ili kuongeza ufanisi.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu anayesimamia TEHAMA katika Sekretarieti ya Ajira Mhandisi Samwel Tanguye amesema changamoto katika mfumo huo zilizojitokeza zilihusu maeneo matatu ikiwemo eneo la kuingiza taarifa Binafsi, Taarifa za Anuani, Taarifa za kielimu sambamba na maeneo mengine ambayo imeonekana kuna umuhimu wa kuyaboresha katika mfumo huo ili kukidhi mahitaji ya wadau ikiwa ni pamoja na watumiaji wa mfumo ili kuleta tija katika  utendaji kazi wa Sekretarieti ya Ajira.

“Tumefanya maboresho katika mfumo wetu ili kukidhi hitaji la wateja wetu lakini pia ikiwa ni hatua ya kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, nitumie fursa hii kuwaomba waombaji kazi ambao tayari wana akaunti kwenye ‘portal’ ya ajira (portal.ajira.go.tz) wapitie akaunti zao na kuboresha taarifa zao hasa katika maeneo matatu ambayo ni eneo la taarifa binafsi, taarifa za anuani na taarifa za kielimu ili kuendana na mabadiliko, amefafanua Tanguye”.

Ameongeza kuwa katika maboresho hayo, mfumo huo hautamruhusu mwombaji kazi mwenye elimu ngazi ya astashahada kuomba kazi ambazo zinawahusu wenye stashahada, mwenye stashahada kuomba kazi zinazowahusu waombaji wenye shahada na pia mwenye shahada hawawezi kuomba kazi zinazohitaji waombaji wenye sifa za stashahada, ama mwenye stashahada hataweza kuomba kazi ya astashahada.

Aidha, maboresho ya Mfumo huo yanawezesha kuwachuja waombaji kazi kulingana na sifa za msingi zilizotolewa katika tangazo la kazi. Kwa mfano endapo moja ya sifa ni umri ama uzoefu, mfumo utawaruhusu wale tu wenye sifa stahiki kuomba kazi hiyo. Pia, endapo tangazo linahusu taaluma “professionals”, basi wasio na “professional” hiyo hawataweza kuomba. Mfano, endapo tangazo linawataka wahasibu wenye CPA, Wahandisi wenye cheti cha Usajili wa bodi ya makandarasi (ERB), Wauguzi wanaopaswa kuwa na cheti ya Bodi ya Wafamasia na Taaluma nyingine zinazofanana na hizo kama hawana vyeti hivyo hawataweza kuomba kazi hiyo.

Sambamba na hayo, kupitia maboresho yaliyofanyika mfumo unaweza kumruhusu mwombaji kazi ambaye amepoteza vyeti vyake na hakuwa na nakala za vyeti vyake kuomba nafasi za Ajira pasipo usumbufu. Kinachotakiwa kwake ni kuwa, sharti awe ametoa taarifa baraza la mitihani na Sekretarieti ya Ajira  kupata uthibitisho wa elimu yake kutoka taasisi husika kama vile Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) au Taasisi nyingine inayohusika kulingana na cheti husika.

Aidha, Maboresho hayo katika mfumo wa ajira yatamuwezesha muombaji kazi anayetuma maombi ya kazi kupitia mfumo kuweza kupata mrejesho wa aina mbili kama ifuatavyo;

Mrejesho wa kwanza ni pale mwombaji anapoomba kazi ambayo hakustahili kuiomba kutokana na sifa zilizopo katika tangazo. Mfumo hautamruhusu kuomba kazi hiyo na utampa sababu ya kutokustahili. Mfano, endapo tangazo linamhitaji mwombaji awe na umri chini ya miaka 45, wale wote ambao umri umezidi hawataruhusiwa kuomba na mfumo utawapa sababu ya kutokubaliwa kuomba kazi hiyo kwa kuwa na umri mkubwa.

Pili, mrejesho kupitia akaunti ya mfumo na barua pepe (email). Katika hatua hii  mwombaji kazi baada ya kufanikiwa kuomba kazi, atakuwa anapokea mrejesho kulingana na hatua “stage” ya usaili iliyopo. Mathalani, akiomba kazi na kufanikiwa, mfumo utamtumia barua pepe ukimjulisha kuwa maombi yako yamefika na akichaguliwa ‘shortlisted’ mfumo utamjulisha kuwa amechaguliwa kwa hatua nyingine na hata anapofaulu usaili, mfumo una uwezo wa kumjulisha kuwa amefaulu usaili.

Kwa upande wake Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amesema kuwa maboresho katika mfumo wa maombi ya kazi maarufu kama ‘Recruitment Portal’ yamesaidia kuendelea kupunguza muda wa uendeshaji wa mchakato wa ajira ambapo kwa sasa mchakato huo unatumia siku 52 lakini kupitia maboresho hayo muda huo utapungua zaidi, lengo ikiwa ni kufikia siku 42 ama pungufu ya hapo.

Ameongeza kuwa maboresho hayo yameufanya mfumo uweze kubaini waombaji kazi ambao hubadilisha taarifa zao ili kuomba kazi ambapo hatua hii itasaidia kuweka kumbukumbu ya kila badiliko linalofanywa na mwombaji kupitia akaunti yake na hivyo ni rahisi kuwabaini waombaji kazi wadanganyifu.

Mwisho, amewataka wadau wote wanaopenda kufanya kazi Serikalini na wana sifa kujisajili kwenye mfumo kwa wakati na kuwasilisha maombi ya kazi pindi nafasi za kazi zinapotangazwa kupitia mfumo wa ajira “portal.ajira.go.tz”. Endapo watakumbana na changamoto yoyote ya kimfumo Ofisi za Sekretarieti ya Ajira ziko wazi wasisite kuwasiliana nao ili kupata huduma stahiki.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma tarehe 27/03/2018.