WATUMISHI WA SEKRETARIETI YA AJIRA WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

WITO umetolewa kwa Watumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma  kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma huku wakikumbuka dira na dhima ya Taasisi wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Akiongea katika kikao cha Wafanyakazi, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Bw. Xavier Daudi amewaeleza watumishi hao kuwa ni muhimu wakajitathimini kila mmoja namna anavyofanya kazi na kujiwekea malengo binafsi yatakayomsaidia kujipima alivyoweza kutekeleza. Ambapo amewasisitiza kutambua Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imepewa dhamana kubwa na Serikali ya kutafuta Rasilimali watu, hivyo ni muhimu kuitunza dhamana hiyo kwa uangalifu.

Pia, amewasisitiza watumishi hao kuendelea kuwa waaminifu katika utendaji kazi ili kuiwezesha Serikali kupata watumishi watakaoweza kutekeleza Mkakati wa Maendeleo wa Taifa na kuifikisha nchi katika uchumi wa kati.

“Nawasihi watumishi wenzangu kutambua kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inaongozwa kwa dhana nzima ya utendaji kazi wenye tija na Uaminifu kazini, kila mtu ahakikishe anafuata misingi hiyo kwenda kinyume na hapo ni kurudisha nyuma maendeleo yanayotakiwa na Serikali” Alisisitiza Daudi.

Akielezea mafanikio ya kiutendaji ndani ya Sekretarieti ya Ajira Daudi amesema mageuzi yanayoendelea ya kielektroniki ikiwemo matumizi ya Mfumo wa uombaji kazi kwa njia ya mtandao, mbali na kusogeza huduma kwa wadau, imerahishisha mchakato wa ajira na kuondoa urasimu na upendeleo ambapo hivi sasa kila Mtanzania mwenye sifa na vigezo stahili anaweza kupata kazi serikalini bila ya kumjua mtu yeyote.

Katika kikao hicho mada nne ziliwasilishwa kwa lengo la kukuza uelewa katika masuala mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa watumishi hao.

Mada hizo ni kuhusu Mfumo wa mawasiliano ya ndani (intranet), Marekebisho ya Kanuni za Uendeshaji wa Shughuli za Sekretarieti ya Ajira, nyingine ni kuhusu masuala ya Itifaki na Huduma kwa Mteja pamoja na mafunzo kuhusu Taratibu za Ununuzi na Usimamizi Mali.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxmwishoxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *