TAHADHARI NA MATAPELI WA AJIRA

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inatoa tahadhari kwa wadau wake kujihadhari na matapeli wanaowapigia simu kwa kutumia majina ya baadhi ya Viongozi wa Taasisi kuwaomba rushwa ya fedha ili kuweza kuwasaidia kupata ajira serikalini.

Sekretarieti ya Ajira inatoa tahadhari hii baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya waombaji kazi ambao wamedai  kupigiwa simu na watu wanaojitambulisha kwa kutumia majina ya baadhi ya Viongozi wa Sekretarieti ya Ajira na kuwadai kiasi cha fedha kama sharti ya kuwasaidia katika mchakato wa ajira na hatimaye kuweza kupata nafasi ya kazi.

Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma haina utaratibu wa kuomba fedha au zawadi ya aina yeyote kwa waombaji wa nafasi za kazi kama sharti la kupata kazi serikalini. Ni vyema ikaeleweka wazi kuwa  Uendeshaji wa Mchakato wa Ajira Serikalini unazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu na unaendeshwa kwa uwazi kuanzia hatua ya kutoa tangazo la kazi, tangazo la kuitwa kwenye usaili na tangazo la kuwapangia kituo cha kazi na si vinginevyo.

Aidha, tunatoa angalizo kwa wadau wetu wote kuwa makini katika kujiunga na baadhi ya mitandao ya kijamii ikiwemo kujaza taarifa zao binafsi ambapo wakati mwingine huwezesha matapeli wa mitandao (hackers) kupakua taarifa hizo na kuitumia kufanya utapeli kwa waombaji kazi, hii ni pamoja na wale wanaotumia huduma za kompyuta za (Internet Café) wakumbuke kufuta ama kuchukua nyaraka na vifaa vya kunakilia taarifa walivyokwenda navyo, pindi  wanapomaliza kazi ili kuepuka watu wasiohusika kupata taarifa zao.

Wakati huu, Ofisi yetu ikiendelea na uchunguzi wa kuwabaini matapeli hao ili kuwachukulia hatua za kisheria, tunaamini wadau wetu wataongeza umakini na kuchukua tahadhari na watu wa namna hiyo.

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma

16 Septemba, 2019

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *