WATUMISHI WATAKIWA KUJITATHMINI KWA UPYA KATIKA UTENDAJI KAZI WAO

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amewataka Watumishi wote wa Sekretarieti kujitathmini na kukumbuka dhima na malengo waliyojiwekea  katika utendaji kazi ili kuweza kukidhi matarajio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika Sekta ya Ajira nchini.

Katibu amesema hayo wakati wa mafunzo ya mfumo wa ajira yaliyotolewa kwa Watendaji wa Sekretarieti ya Ajira leo jijini Dar es Salaam na kuwakumbusha watendaji hao baadhi ya maazimio waliyokuwa wamejiwekea katika kutimiza majukumu yao akisisitiza umuhimu wa kutambua matarajio makubwa waliyonayo wananchi katika Taasisi hiyo.

Aidha, alieleza kuwa ni zaidi ya miaka kumi sasa tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo kwa mujibu wa Sheria ambapo mapinduzi makubwa yamefanyika katika sekta ya ajira nchini. Ameyataja baadhi ya mapinduzi hayo kuwa ni pamoja na kufanikiwa kupunguza gharama kwa Serikali na kwa waombaji wa nafasi za kazi, pia wameongeza ufanisi ikiwemo wa matumizi ya TEHAMA katika kuendesha mchakato mzima wa Ajira, jambo lililowasaidia kufikia wadau wengi kwa  urahisi.

Hata hivyo, aliongeza licha ya mapinduzi hayo ni muhimu kwa watumishi hao kujitafakari wanajionaje na jamii inawaonaje ili kuweza kusahihisha maeneo ambayo wanaona hayaendi  sawa kiutendaji.

“Ni vema tukajitafakari, sisi tunajionae na watu wanatuonaje? Je Taasisi yako unaipa nini cha ziada, na zile changamoto tunazozipata ni vizuri tukazitumia kama fursa na kubadilika kiutendaji pale panapohitaji kufanya hivyo?” Alieleza Katibu.

Pamoja na hayo aliwataka watumishi hao kufanya kazi kwa umoja na upendo kwa kuzingatia umuhimu wa kila kitengo na Idara katika kuhakikisha azma ya Serikali ya kurahisisha zoezi zima la upatikanaji wa ajira katika Utumishi wa Umma kwa watu wenye sifa linafikiwa.

Akizungumzia juu ya mifumo ya Ajira inayotumika alisema Sekretarieti Ajira imefanikiwa kuwa na mifumo bora inayozungumza na mifumo mingine ya utambuzi ambayo pia imesaidia katika uhakiki wa taarifa muhimu za wadau wanaoomba fursa za ajira. Baadhi ya mifumo hiyo ni pamoja na NIDA, NECTA na NECTA. Na kwa sasa Sekretarieti ya Ajira ipo katika mchakato wa kuunganisha na mfumo wa kiutumishi (HCMIS).

Naye Mkuu wa Idara ya TEHAMA, Mhandisi Samwel Tanguye amesema mafunzo hayo yametolewa kwa Waajiri nchi nzima kikanda ambapo yamefanyika katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam. Mafunzo hayo yameshirikisha jumla ya washiriki 661. Kati yao Wizara zilizoshirikishwa zilikuwa 20, Taasisi za Umma 127, Sekretarieti za Mikoa 25 na Mamlaka ya Serikali za Mitaa 183.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxMWISHOxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *