WAAJIRI NCHINI WATAKIWA KUAJIRI WATU WENYE SIFA SERIKALINI

WITO umetolewa kwa Waajiri wa Taasisi za Umma na Sekretarieti za Mikoa nchini kutumia vizuri mfumo wa maombi ya kazi ili kuhakikisha wanaisaidia Serikali wakati wa mchakato wa Ajira wanaajiri watu wenye sifa na vigezo vinavyotakiwa serikalini kwamujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Bw. Xavier Daudi alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waajiri  wa  mikoa ya Morogoro, Lindi , Pwani, Dar es Salaam  na Mtwara yaliyofanyika jijini Dar es salaam katika ukumbi wa chuo cha Utumishi wa Umma leo. Mafunzo hayo yalilenga kutoa elimu kwa waajiri ili waweze kufahamu kazi zote wanazopaswa kuzifanya katika mfumo huo.

Katibu alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya tano inalengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda, na ili lengo hili litimie linahitaji watumishi wenye vigezo, weledi, na maadili mema na huwezi kupata watumishi wanaostahili kama mifumo hii ya kuchuja haitatumika vizuri.

“ni vizuri sote tukatambua  mtu anapoajiriwa na  Taasisi au Halmashauri  fulani ni  Mtumishi wa Umma na ataweza kufanya kazi sehemu yoyote atakayopangiwa na Serikali, hivyo endapo sote tutazingatia Sheria na misingi tunayopaswa kuzingatia bila ya kuwa na upendeleo, Serikali itapata watumishi wale wanaostahili tu na si vinginevyo” Alisisistiza.

Akielezea kuhusu mfumo wa Ajira jinsi ulivyo amesema mfumo unaotumika hivi sasa umeshaunganishwa na mifumo mingine ya utambuzi ili kusaidia kupata uhakika wa taarifa za mwombaji, ambapo ameainisha mifumo hiyo kuwa ni pamoja na NIDA, NACTE na RITA.

Aidha, alifafanua kuwa mfumo huu ukitekelezeka vizuri utakuwa ni wa haraka na  nafuu kwa watumiaji kwani mchakato mzima wa ajira unategemewa kutumia siku 40 tu ukilinganisha na hivi sasa ambapo tumekuwa tukitumia zaidi ya siku 90. Mbali na hayo amesema mfumo huu  kwa kiasi kikubwa utapunguza changamoto zilizokuwa zinajitokeza katika eneo la ajira na hii itapelekea dhamira ya Sekretarieti ya Ajira kuwa kituo cha umahiri kutimia.

“ili haya yote yaweze kukamilika ni muhimu kwa Maafisa Utumishi kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Maana sisi kukabidhiwajukumu la kuendesha mchakato wa ajira ina maana tumeaminika na inapaswa tutambue dhamana hiyo na kuitekeleza kwa weledi” alisisitiza Daudi.

Aidha, aliwataka waajiri baada ya kupata mafunzo hayo wawe mabalozi wazuri kwa kuanza kutumia mfumo huo ili kumuwezesha mlipa kodi aweze kufurahia huduma za Serikali. Alisisitiza kuwa ni lazima waajiri wawe mawakala wa mabadiliko kwani Serikali yetu inaenda kwa kasi sana hivyo basi ni muhimu kuendana na mabadiliko hayo.

“Tujitahidi kutumia mfumo huu ili uwe kati ya mambo mazuri yatakayoweza kutangazwa katika Serikali ya Awamu ya Tano. Tumsaidie Mhe. Rais kutangaza mambo mazuri ya Serikali yanayofanyika nyie mpo karibu na wananchi tafadhali zingatieni hilo” Alisisitiza.

Naye Naibu Katibu Idara ya TEHAMA Mhandisi Samuel Tangue alieleza kuwa mafunzo hayo yamelenga Waajiri wote katika Sekta ya Umma nchini ili kuwawezesha kuwa na uelewa wa kutosha kuweza kutumia mfumo huu kwa maombi ya kazi na kuendesha mchakato mzima wa Ajira nchini kwa ufanisi.

Sekretarieti ya Ajira imeendesha  mafunzo ya Mfumo wa Ajira kwa kugawa kikanda ambapo mafunzo haya yanatarajiwa kumalizika kwa makundi yote ya Waajiri ndani ya wiki mbili zijazo. Mafunzo haya yalifunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Kapt. George Mkuchika jijini Dodoma.

 

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXMWISHOXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *