SEKRETARIETI YA AJIRA YATUMIA CHANGAMOTO KAMA FURSA YA KUBORESHA HUDUMA

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Xavier Daudi amesema kuwa Ofisi yake ilitumia changamoto ya malalamiko ya wadau kuwa fursa ya kuboresha huduma zake, baada ya kujitathmini na kuamua kubadilika kwa kuwa wabunifu kwa kutumia TEHAMA walianzisha mifumo mbalimbali ikiwemo mfumo wa maombi ya kazi unaojulikana kama (Recruitment Portal).

Daudi amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya Waajiri wa Taasisi za Umma zilizopo jijini Dar es Salaam. Alibainisha kuwa baada ya kupokea malalamiko kadhaa kutoka kwa wadau wake kuhusu uendeshaji wa mchakato wa ajira, ofisi yake iliamua kujitathmini na kuona baadhi ya changamoto zinazolalamikiwa zinatokana na njia wanazotumia katika kutekeleza majukumu yake na hivyo kuamua kubadilika.

Akiainisha baadhi ya malalamiko waliyokuwa wakiyapata kuwa ni pamoja na mchakato wa ajira kuchukua muda mrefu, baadhi ya maombi ya kazi kutowafikia kwa wakati, matangazo ya kazi kufikia watu wachache, baadhi ya waombaji kutopata mrejesho, mlundikano wa karatasi za maombi ya kazi pamoja na gharama kubwa za kutoa matangazo zilizokuwa zikiwakabili wenyewe.

Daudi alibainisha faida za kutumia mfumo kwa upande wa Waajiri na kusema kuwa mfumo utarahisisha baadhi ya majukumu yao ikiwemo uhifadhi wa taarifa, gharama kubwa za kutoa matangazo, sehemu ya kuhifadhi nyaraka, maana mfumo utamwezesha Mwajiri akishapata kibali ataingiza mwenyewe kibali hicho katika mfumo, kuliko ilivyo hivi sasa mpaka akitume au kukipeleka mwenyewe Sekretarieti ya Ajira.

Akatolea mfano baada ya mchakato kukamilika na waliofaulu usaili kupangiwa kituo Mwajiri ataweza kuona moja kwa moja akiwa ofisini kwake na pia atapata taarifa na nyaraka za mwombaji aliepangiwa bila ya kusafiri au kusubiri zitumwe, jambo ambalo litamwezesha kuendelea kujiridhisha na taarifa za mwombaji aliyefaulu usaili hata kabla hajaripoti kazini na atakaporipoti inabaki kukamilisha taratibu.

“pamoja na hayo niliyoyasema ningependa mfahamu kuwa mfumo huu wa maombi ya kazi umeunganishwa tayari na mifumo mingine, hivyo utawawezesha kutoa mrejesho kwa wadau, ikiwemo kuhakiki taarifa za wasailiwa, matokeo ya kitaaluma NECTA, NACTE pamoja na taarifa binafsi kupitia Mfumo wa kuchangia taarifa za utambulisho wa taifa (NIDA), ni dhahiri kwa utaratibu huu watakaoajiriwa watakuwa ni Watanzania wale tu wenye sifa za kuwa Watumishi wa Umma” amesema Daudi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Idara ya Ajira katika Sekretarieti ya Ajira, Bw. Lucas Mrumapili amesema mfumo huo wa maombi yakazi mbali ya kuokoa gharama kubwa kwa Serikali na kwa Waombaji kazi, pia umeboresha utendaji kazi na kupunguza baadhi ya changamoto zilizokuwa zikiwakabili

Akitolea mfano kwa waombaji kazi amesema hivi sasa wataweza kupokea mrejesho wa wakati ikiwemo kupokelewa kwa maombi ya kazi, kuchaguliwa kwa ajili ya usaili ama kutochaguliwa na sababu ya kutochaguliwa, atajulishwa endapo amefaulu usaili na kupangiwa kituo cha kazi. Sambamba na hayo utawapunguzia gharama za kutoa nakala za mara kwa mara kwa ajili ya kuwasilisha maombi ya kazi, maana hivi sasa hayo yote wanaweza kupata kiganjani.

Pia, alibainisha faida nyingine watakayoipata waombaji wa fursa za Ajira waliopoteza vyeti vya elimu ya Sekondari hivi sasa watatakiwa kufahamu namba ya mtihani na mwaka waliohitimu shule na kuiingiza na matokeo yao kwenye mfumo na watapa taarifa husika papo hapo.

Mafunzo hayo ya siku mbili, yanaendeshwa na Sekretarieti ya Ajira, yameshirikisha baadhi ya Wakurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu na wasaidizi wao katika Taasisi mbalimbali za Umma ikiwa ni muendelezo wa mafunzo kwa Waajiri wa sekta za Umma nchini ambayo yalizinduliwa rasmi mwisho mwa mwezi Mei mwaka huu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Kapt. Mstaafu George Mkuchika jijini Dodoma.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxENDxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *