HOFU YA MUNGU IMEMSAIDIA KUSTAAFU SALAMA SERIKALINI

Hayo yamesemwa na Bi Atuganile Mwaigomole ambae amestaafu hivi karibuni wakati wa hafla fupi ya kumuaga iliyoandaliwa na umoja wa wanawake wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, iliyofanyika ofisini hapo jana.

Bi. Mwaogomole amesema kutokana na kazi yake yakushika fedha aliyoifanya kwa zaidi ya miaka thelathini (30) serikalini kama angekuwa hana hofu ya Mungu, leo hii asingekuwa anaagwa na wenzake bali angekuwa jela.

Ambapo alitumia nafasi hiyo kuwataka wanawake hao kuendelea kuwa na hofu ya Mungu, kuchapa kazi, kuwa watii, kutimiza wajibu na kuwa na upendo kwa watu wote.

“Naomba niwaeleze wanawake wenzangu ukweli ni kwa neema ya Mungu nimeweza kufikia siku ya leo nikistaafu salama, lakini siri ya mafanikio yangu ni kusali, utii, upendo, ushirikiano, kujituma na kutokuwa na tamaa” alifafanua Bi.Mwaigomole.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa umoja wa wanawake wa Sekretarieti ya Ajira Bi Doroth Ndabi pamoja na kumpongeza Bi Mwaigomole kwa upendo, ucheshi na ushirikiano aliokuwa nao ndani ya taasisi, pia aliwataka wanawake wenzake kumuenzi mwenzao aliyestaafu kwa kuwa na ushirikiano na kuchapa kazi ili na wao wakijaliwa kustaafu waweze kuagwa vizuri na kukumbukwa kwa mema waliyoyafanya.

Nae Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu katika Sekretarieti ya Ajira Bi Victoria ambae ni miongoni mwa umoja huo, amesema yeye alipata bahati ya kufanya kazi muda mrefu na Bi Mwaigomole tangu wakiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, lakini kote huko Bi Mwaigomole amekuwa na mvumilivu, mchapakazi, mwaminifu pamoja na kufanya kazi eneo nyeti lenye vishawishi vingi.

Nao wanawake wa Sekretarieti ya Ajira kwa pamoja wamemwahidi Bi Atuganile Mwaigomole kutomwangusha na badala yake wataendelea kuwa mabalozi wazuri kiutendaji ndani na nje ya taasisi hiyo na kwa jamii inayowazunguka.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxmwishoxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *