WAOMBAJI WA FURSA ZA AJIRA SERIKALINI WATAKIWA KUWA NA KITAMBULISHO CHA TAIFA IFIKAPO MWISHONI MWA MWEZI JULAI 2019

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw Xavier Daudi amewataka waombaji wote wa fursa za Ajira Serikalini kuhakikisha wanafuatilia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kuweza kupata kitambulisho hicho cha Taifa ambacho kitakuwa ni kigezo kimojawapo kitakachomwezesha mwombaji wa nafasi wazi za kazi zitakazotangazwa na Serikali.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, ikiwa ni takribani mwezi mmoja umepita tangu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika alipotoa tamko la kuwataka wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kuhakikisha wanafuatilia kitambulisho cha Taifa kwa kuwa Serikali imeendelea kuboresha mifumo yake ikiwemo Mfumo wa maombi ya kazi kupitia Sekretarieti ya Ajira ujulikanao kama (Recruitment Portal), wakati akizindua mafunzo ya Waajiri katika sekta za Umma nchini jijini Dodoma.
Mhe. Mkuchika alisema kuwa mfumo huo wa maombi ya kazi uliobuniwa na Sekretarieti ya Ajira umeunganishwa tayari na mifumo mingine kutoka taasisi za NECTA na NACTE ili kurahisisha uhakiki wa taarifa za waombaji kazi. Pia Mfumo huu umeunganishwa na Mfumo unaosimamiwa na NIDA ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi. Kutokana na kuungana kwa mifumo hii muhimu ya Serikali ni dhahiri watakaoajiriwa watakuwa ni Watanzania wenye sifa za kuwa Watumishi wa Umma.
Waziri Mkuchika aliitaka Sekretarieti ya Ajira ambayo ni chombo chenye dhamana ya kuendesha mchakato wa Ajira kwa niaba ya Waajiri katika Utumishi wa Umma na Waajiri wote waliokasimiwa jukumu la kuendesha mchakato wa Ajira nchini kuhakikisha inatumia mfumo wa maombi ya kazi kwa kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha (2019/20) waombaji wa fursa za ajira wanaoweza kuajiriwa Serikalini ni wale tu wenye kitambulisho cha Taifa baada ya kukidhi vigezo vingine ikiwemo vya kitaaluma ili kuepuka kuajiri watu wasiostahili.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira amewasisitiza Watanzania wote hususani wale wenye nia ya kuomba kazi Serikalini kuhakikisha wanatumia muda uliotolewa na Serikali kuhakiki watumiaji wa simu za mkononi kujisali Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ili waweze kupata namba ya kitambulisho ama kitambulisho chenyewe mapema iwezekanavyo maana Ofisi yake itaanza kutekeleza agizo la Serikali lililotolewa na Waziri Mkuchika kuanzia mwezi Agosti mwaka huu.
“Nisingependa kumwona Mtanzania yeyote mwenye sifa za kitaaluma za kuomba nafasi wazi ya kazi zitakazotolewa na Serikali anashindwa kuomba kutokana na kukosa namba ya kitambulisho cha Taifa” amesema Daudi.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxMWISHOxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *