Sekretarieti ya Ajira inawataka wadau kutumia Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma kupata huduma zaidi

Wadau wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma wametakiwa kutumia fursa iliyotolewa na Serikali ya kuwa na Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutembelea Ofisi za Sekretarieti ya Ajira ili waweze kupata ufafanuzi juu ya jambo lolote linalowatatiza kuhusu uendeshaji wa Mchakato wa Ajira za Utushimi serikalini.
Msemaji wa Sekretarieti ya Ajira Bi Riziki Abraham amesema hayo leo alipokuwa akiongea na baadhi ya wadau waliomtembelea ofisini kwake wakitaka kupata ufafanuzi wa masuala ya Ajira katika Utumishi wa Umma, ambapo amebainisha kuwa pamoja na huduma wanazozitoa kila wakati ila kipindi hiki wametenga nafasi maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wadau wote wanaopenda kufahamu lolote kuhusu Ofisi hiyo.
“Unapoongelea Ajira unaongelea maisha ya watu, hivyo, kutokana na umuhimu huo, Ofisi imeamua kutenga siku ya tarehe 17 mpaka 20 Juni kutoa huduma maalum ili wadau waweze kujionea maboresho makubwa ya mifumo kupitia TEHAMA hasa ukizingatia kaulimbiu ya mwaka huu inahusu vijana na matumizi ya Teknolojia, hivyo ninawaomba wadau wote wenye kutaka kufahamu lolote kuhusu mchakato wa Ajira serikalini wasisite kutembelea Ofisi zetu za Dar es Salaam na Zanzibar ili wapate kilicho bora na si bora huduma” amefafanua Msemaji huyo.
Aidha, Bi Riziki amesema Sekretarieti ya Ajira pamoja na kutoa huduma kwa wadau pia itajishughulisha na shughuli za kijamii ikiwemo kufanya usafi katika maeneo ya Ofisi na maeneo jirani ya ofisi hizo katika kituo cha huduma za usafiri Kivukoni katika kipindi cha Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma.
Maadhimisho haya yameaanza rasmi tarehe 16 mwezi huu yanatarajiwa kumalizika tarehe 23 Juni, 2019, yakiwa na Kaulimbiu inayosema “uhusiano kati ya uwezeshaji wa Vijana na usimamizi wa masula ya uhamiaji, kujenga utamaduni wa utawala bora, matumizi ya TEHAMA na ubunifu katika utoaji wa huduma jumuishi”.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxMWISHOxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *