TEHAMA yarahisisha mchakato wa Ajira serikalini

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imezidi kuboresha huduma zake kwa kuanza kuendesha usaili wa mahojiano kwa njia ya mtandao (Video Conference) baada ya usaili wa kwanza kufanyika wiki hii kwa  baadhi ya nafasi za Watendaji Waandamizi ambapo mmoja wa wasailiwa alikuwa mkoani Mbeya na wajumbe wa jopo la usaili wakiwa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Wajumbe wa jopo la Usaili huo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Bw Waziri Kindamba amesema kuwa Sekretarieti ya Ajira ni  miongoni mwa Taasisi za Serikali zilizoamua kufanya mageuzi katika kuhakikisha inaboresha huduma zake kwa wadau ili kuweza kuwafikia popote pale walipo kwa kutumia teknolojia katika mawasiliano.

Amebainisha kuwa hatua waliyoichukua Sekretarieti ya Ajira ni jambo la kuigwa na taasisi nyingine, kwanza kwa kuwa wabunifu, pili kuokoa muda na gharama kwa wasailiwa kusafiri na mwisho kuonyesha uzalendo kwa kutambua na kuamua kutumia miundombinu ya TTCL kuendesha usaili wake kwa waombaji kazi walioko nje ya Dar es Salaam.

Kwa upande wake Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amesema kuwa taasisi yake imejipanga kuhakikisha inasogeza huduma karibu na wadau wake ikiwemo kurahisisha mchakato wa Ajira kwa lengo la kuongeza ufanisi.

“Sekretarieti ya Ajira imeshafanya maboresho mengi tangu tulipokabidhiwa jukumu hili la kuendesha mchakato wa ajira serikalini, awali tulianza kwa kwa waombaji kazi kutuma maombi yao kwa njia ya posta na badae tukabadilisha na kuanza kupokea maombi kwa njia ya mtandao, kwa sasa tumejikita zaidi katika matumizi ya TEHAMA, kwa kuanzisha mifumo mbalimbali ili kurahisisha utendaji wa kazi na kuongeza ufanisi” amesema Daudi.

Daudi amefafanua baadhi ya mifumo hiyo kuwa ni pamoja na mfumo wa wa kuendesha usaili kwa njia ya mtandao (video conference), mfumo ya upokeaji wa maombi ya kazi (Recruitment portal), mfumo wa kupanga wasailiwa waliofaulu usaili (Placement Management Information System) na mfumo wa kutoa taarifa kwa waliopotelewa na vyeti mbalimbali vya kitaaluma (Loss report management system) wakishakamilisha taratibu.

Aliongeza kuwa nia ya Sekretarieti hiyo kuendelea kubuni mifumo inalenga  kuongeza ufanisi, kupunguza muda wa kufanya mchakato wa ajira kutoka siku 90 hadi siku 52 kwa ajira mpya na kwa wale wanaohifadhiwa katika kanzidata kutumia muda wa wiki moja kwa mwajiri kupata mtumishi anayemuhitaji. Hatua hii inalenga kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi na kupunguza malalamiko ya ucheleweshaji wa michakato ya ajira na kuondoa hisia za upendeleo kwa kuwa anayepata kazi ni yule mwenye sifa na vigezo stahili na si vinginevyo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

11 Comments

 1. Agrey Moshi

  Naomba kuongeza pia , kwa upande wa written interviews napenda pia kutoa mchango wa uboreshaji kama inawezekana kungekuwa na system ya kufanya mtihani online/ mtandaoni maana hiyo imekua changamoto kubwa kwa watu kutumia nauli kutoka mbali kwaajili ya written interview. Nazan mtihani wa online unawezekana maana mfumo ukipangiliwa vzuur utakua na limit/ukomo katika kujibu kila swali yaan dakika au muda kadhaa kwa kila jibu ili kuweka supervision au namna yoyote ile lakini iwe inasimama badala ya msimamizi, maana yangu n kwamba endapo mtu atajua kuwa sasa nimepita katika mtihani nimeitwa kwenye usahili wa mahojiano itakua rahisi kwa yeye hata kutumia nauli kuja Dar es salaam sasa. Hiyo nazani ingesaidia kupunguza gharama kwenu pia kwa waombaji ya kusafiri huku na kule kwaajili ya mtihani badala yake mtu anakosa nafasi sehem hata 7 au 3 ambazo amesafiri na ametumia gharama nauli, malazi, chakula, ila angepata uhakika kabla hajasafiri kuwa nimepita mtihani( kwa huo mfumo wa online test ambao utampa majibu akiwa hukohuko alipo kwa njia ya email) ndipo aje kwaahili ya usahili wa mahojiano.
  Ahsanteni

  Reply
  1. PSRS (Post author)

   Asante Moshi tumeyapokea maoni yako

   Reply
   1. Agrey Moshi

    Ahsante,

    Reply
 2. SHAHA CHANG'A

  you deserve better where you reached! it a tremendous and brilliant development…..congrats PSRS

  Reply
  1. PSRS (Post author)

   Thank you Mr Shaha

   Reply
 3. Festo Ngonela

  Pongezi kubwa kwahatua hii ya kufanya usaili kwa video conference hakika itatupunguzia gharama kwa sisi tulio mikoani.

  Reply
  1. PSRS (Post author)

   Tunashukuru kwa pongezi, tunaendelea kuboresha huduma zeti ili ziweze kuwafikia wananchi kwa urahisi na gharama nafuu

   Reply
 4. MwanaAfya

  Hii ni nzuri sana na mtaokoa gharama nyingi sana kwa watanzania.
  Mimi mdau wa technology, kwa hili nawapongeza.

  Ushauri: Kwa wale ambao mshawafanyia usaili na wakafaulu ila hawakupata nafasi si vyema kuwasaili tena Bali mwapangie kazi Mara tu mpatapo nafasi ya kazi inayomhusu.

  Reply
  1. PSRS (Post author)

   Asante kwa ushauri wako MwanaAfya

   Reply
 5. Godfrey Kisanga

  Tunashukuru kwa kuwepo kwa hii huduma ila bado inachukua mda mrefu tangu kutuma form za maombi ad kuitwa kazini. Mm nilikua naomba kwa kua inachukua muda mrefu bas wangekuwa wanatoa tarehe kua tarehe flani ndo labda majina ya watakao itwa kweny interview yatawekwa so itatupunguzia usumbufu wa kila siku kuweka vocha na pia kumiss interview

  Reply
  1. PSRS (Post author)

   Asante Kisanga, tumepokea maoni yako

   Reply

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *