Sekretarieti ya Ajira yapongezwa kwa kuanzisha mifumo ya Ajira.

Sekretarieti ya ajira katika Utumishi wa Umma imepongezwa kwa jitihada inazoendelea kufanya katika maboresho ya mchakato wa ajira hasa kubuni mfumo ya upokeaji wa maombi ya kazi na mfumo wa kupanga wasailiwa waliofaulu usaili.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa mwishoni mwa wiki alipokutana na Bodi, Watendaji na watumishi wa Sekretarieti hiyo kwa lengo la kuzitembelea taasisi zilizo chini ya Ofisi yake ili kujua wanavyotekeleza majukumu waliyokabidhiwa na kufahamiana na watendaji wake.

“Nataka mtambue chombo hiki kimeanzishwa ili kutekeleza majukumu yake kwa uwazi na kutenda haki kwa kuzingatia kuwa Serikali ya awamu ya tano inandelea kupata Watumishi wa Umma wenye sifa, weledi na maadili mema,” alisisitiza Naibu Waziri.

Sambamba na hilo amewapongeza kwa kuanzisha mifumo ya kupokea maombi ya kazi na mfumo wa kuwapangia waombaji waliofaulu usaili huku akiamini kuwa mifumo hiyo imeongeza uwazi na kupunguza malalamiko ya ucheleweshaji wa michakato ya ajira na kuondoa hisia za upendeleo kwa kuwa hivi sasa atakayepeta ajira ni yule mwenye sifa na vigezo vinavyostahili.

Dkt Mwanjelwa aliongeza kuwa ni vyema elimu kwa umma iendelee kutolewa ili wadau wafahamu namna huduma zilivyoboreshwa ikiwemo kupunguza muda wa kufanya mchakato wa ajira kutoka siku 90 hadi siku 52 kwa ajira mpya na kwa wale wanaohifadhiwa kwenye kanzidata kutumia muda wa siku saba pekee kwa mwajiri anakuwa kupata mtumishi anayemuhitaji.

Alihitimisha kwa kuwataka watendaji wa sekretarieti ya Ajira kuendelea kuchapa kazi kwa kuzingatia uzalendo, maadili ya Utumishi wa Umma kwa kuwa wao ndio wanaopaswa kuwa mfano wa kuigwa na wale wanaowaajiri.

Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira amesema tangu kuanzishwa kwa chombo hicho hadi tarehe 17Januari 2019 wametangaza nafasi 29,291 kwa ajili ya Wizara, Idara, wakala, Sekretarieti za mikoa, Manispaa, halmashauri na Taasisi za Elimu ya Juu. Ambapo jumla ya maombi 1,104,513 yalipokelewa kati yao waombaji 376, 689 waliitwa kwenye usaili na 28,580 wameshapangiwa vituo vya kazi ambapo nafasi 711 ambavyo vibali vyake vimepokelewa hivi karibuni mchakato wake upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya sekretarieti ya Ajira, Bw. Mbarak Abdulwakil kwa niaba ya Wajumbe wenzake na Watendaji wa taasisi hiyo amemshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa nasaha zake na kumuahidi kuwa wataendelea kutekeleza majukumu ya chombo hicho kwa wakati na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu ili taifa liendelee kupata watumishi wenye bora.

Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *