WATUMISHI WA SEKRETARIETI YA AJIRA WATAKIWA KUENDELEA KUZINGATIA MAADILI.

Watumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili waliyojiwekea na kutambua kuwa wao ni kioo cha waombaji kazi wanaoajiriwa Serikalini kupitia Sekretarieti hiyo, hivyo ni wajibu wao kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, Sheria, Kanuni na Taratibu ili hata wale wanaowahudumia wanapoajiriwa wawe watumishi bora wanapoajiriwa.

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Bw. Xavier Daudi amesema hayo leo wakati wa kikao cha pamoja na wafanyakazi wa ofisi hiyo ambapo amewataka watumishi hao kuwa mabalozi wazuri kwa kuchapa kazi na kubadilika wakitambua kuwa kila mtumishi atapimwa kutokana na utendaji kazi wake na si vinginevyo.

“Nawataka mtambue kuwa nyie ndio mabalozi wa Sekretarieti ya Ajira, na balozi mzuri ni yule anayezingatia weledi na kutimiza wajibu wake kwa kufuata misingi ya Sheria, Kanuni na Taratibu akitambua yeye ni kioo cha wale anaowahudumia. Ukiona wewe huwezi kutimiza wajibu wako kwa kufuata maadili basi serikalini sio sehemu sahihi kwako ni vyema ukatafuta pahali pengine” alisema Daudi.

Daudi aliongeza kuwa utofauti wao na watu wengine uonekane katika maadili yao ya kiutendaji ikiwemo uwajibikaji, kujali muda, kuwahi kazini, kutunza siri, kuwa na staha, usawa, ubunifu, kuwa nadhifu na kuheshimu Sheria ili wale wanaowahudumia watamani kufanya kazi Serikalini.

Kwa upande wao watumishi hao waliishukuru Menejimenti ya Taasisi hiyo kwa kuweza kuweka vikao vya pamoja mara kwa mara na watumishi jambo linalochangia kutoa nafasi ya kujadili changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wadau na kwa manufaa ya Taifa.

“Kwa kweli mimi binafsi nimefaidika na mambo mengi ambayo Katibu ametuasa katika kikao hiki ambapo naamini mimi na wenzangu tutaendelea kujituma kwa kuzingatia misingi katika utendaji wetu, maana ni kama ulivyosema taasisi hii inatoa huduma na wengi tunaowahudumia ni vijana wanaotuangalia utendaji wetu, endapo tutafanya kinyume cha maadili yetu hata wao watakosa maadili” alichangia mmoja watumishi

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *