PUBLIC SERVICE RECRUITMENT SECRETARIAT

Taarifa ya Katibu wa Sekretarieti ya Ajira kwa Wahariri PDF Print E-mail
 Taarifa ya Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma katika Mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari na Menejimenti ya Sekretarieti ya Ajira tarehe 24-04-20121.0    Utangulizi

Ndugu Wahariri Pamoja na Wanahabari,
Sekretarieti ya Ajira ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa sheria ili kuendesha mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma na imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kufuata Sheria ya Utumishi wa Umma, Kanuni, Vigezo na Taratibu ilizojiwekea pamoja na  kushirikiana na Wizara na Taasisi za Umma nchini ili kuweza kufanikisha upatikanaji wa Watumishi wa Umma wenye sifa, ujuzi, uzoefu, na maadili yanayohitajika na kwa mujibu wa mahitaji ya Mwajiri.
 
Ndugu Wahariri Pamoja na Wanahabari,
Dira na Dhima ya Sekretarieti ya Ajira.
Dira
Kuwa kituo Bora cha Ajira katika Utumishi wa Umma nchini pamoja na nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.
Dhima
Kuendesha Mchakato wa Ajira kwa kutumia mbinu za Kisasa na kwa kuzingatia Kanuni za Usawa, Uwazi, na Sifa pamoja na kutoa Ushauri kwa Waajiri kuhusu Ajira.

Ndugu Wahariri Pamoja na Wanahabari,
Mfumo wa nafasi  za Ajira katika Utumishi wa Umma.
Utaratibu wa kutangaza na kutuma maombi;
Waajiri wanapaswa kutenga nafasi za Ajira pamoja na bajeti ya mishahara kwa mwaka husika.
Waajiri wanapaswa kupata kibali toka kwa Katibu Mkuu Kiongozi/Katibu Mkuu Utumishi.
Kuhakikisha Tangazo la nafasi za kazi limetolewa katika Vyombo vya Habari kama Magazeti, Tovuti mbalimbali na kuweka katika Ubao wa Matangazo wa Sekretarieti ya Ajira.
Kupokea maombi ya kazi kutoka kwa waombaji kulingana na nafasi husika. Kupitisha posta na sio kuwasilisha moja kwa moja Sekretarieti ya Ajira
Baada ya kupokea maombi ya kazi Sekretarieti ya Ajira huandaa orodha ndefu yaani orodha ya waombaji wote wa nafasi za kazi zilizotangazwa.
Baada ya kuandaa orodha hiyo uchambuzi wa orodha fupi huandaliwa kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa wakati wa kutangaza kazi.  Baada ya kupata orodha hiyo majina hayo huwasilishwa katika kikao cha Sekretarieti ya Ajira.
Kikao cha Sekretarieti ya Ajira kikishapitia orodha fupi waombaji wa nafasi za ajira huitwa katika Usaili kwa kutumia Vyombo vya Habari, Simu, Posta na Wavuti mbalimbali za Waajiri.

Njia zinazotumika na Sekretarieti ya Ajira katika kuchuja ili kubaki na waombaji wenye vigezo kulingana na nafasi za kazi zilizotangazwa.
Kuna aina tatu za michujo ya waombaji kulingana na kada husika kama ifuatavyo;-
Mtihani wa kuandika kwa waombaji wote wenye sifa.
Mtihani wa vitendo (practical) mfano. Mwombaji wa kazi ya Dereva atapelekwa VETA atafanya majaribio ya kuendesha gari au mwombaji wa fani ya Teknolojia ya Habari atapewa Kompyuta na kuambiwa mambo ya kufanya au Mpigapicha atapewa Kamera na kuelekezwa cha kufanya.
Usaili wa ana kwa ana hii ni hatua ya mwisho ya kumpata mwombaji mwenye sifa zinazotakiwa katika nafasi husika.

Pia tunaangalia ubora wa mwombaji ikiwemo kuhakiki vyeti husika alivyowasilisha kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za taaluma pamoja na kupitia vigezo vingine kulingana na nafasi ya ajira iliyotangazwa kama ifuatavyo;-
Tume ya Vyuo Vikuu (Tanzania Commission for Universities – (TCU) ili kuthibitisha uhalali wa cheti na chuo husika alichosoma mwombaji hasa kwa waombaji waliosoma nje ya nchi.
Baraza la Mitihani Tanzania ili kuhakiki uhalali wa cheti husika.
Kuwasiliana na mamlaka nyingine kwa ajili ya uchunguzi ikiwemo wadhamini (referee) waliowasilishwa na mwombaji katika wasifu (CV) wake.

Jukumu na vigezo anavyopaswa kuzingatia Mwombaji wa nafasi ya Ajira katika Utumishi wa umma (Masharti ya Jumla).

Wajibu wa mwombaji wa kazi/Ajira kwanza ni kuzingatia nafasi za kazi zinazotangazwa katika Vyombo vya Habari kama vile Magazeti/Tovuti za Wizara ambazo zimeunganishwa na Ofisi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Mwombaji wa kazi anatakiwa kusoma na  kuzingatia masharti ya Tangazo la kazi kama ifuatavyo:-
Tangazo la kazi ni la aina gani kwa kuangalia kada na vigezo husika (sifa za msingi za kazi husika).

Uraia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kila mwombaji anapaswa kuwa na cheti cha kuzaliwa.

Mwombaji ambaye ni Mtumishi wa Umma ni lazima ajue kuwa kama anaomba kazi baada ya yeye kujiendeleza ni lazima apitishe barua yake kwa mwajiri ili kupata ridhaa ya mwajiri, kutofanya hivyo kunamwondolea sifa ya kuomba kazi.

Mwombaji ambaye tayari ni Mtumishi wa Umma na ameomba kazi ya Cheo cha juu ambayo imetangazwa katika Ofisi ya Serikali ni lazima ajue kuwa anao wajibu wa kupitisha barua ya maombi kwa mwajiri wake.

Mwombaji ambaye tayari ni Mtumishi wa Umma anapaswa kujua kuwa haruhusiwi kuomba tena nafasi kazi katika Utumishi wa Umma kwa nafasi ya kazi inayofanana na aliyoko kwa wakati huo. Mfano, Mtumishi ambaye ni Mchumi daraja la pili katika Wizara fulani na ameona tangazo linahitaji Mchumi Daraja la pili katika Wizara nyingine haruhusiwi tena kuiomba kazi hiyo.
 
Mwombaji ajue kuwa anatakiwa anapoomba kazi aambatanishe na maelezo yake binafsi yaani (CV)

Mwombaji anatakiwa aweke pamoja na maombi yake nakala ya vyeti vya kuhitimu hatua mbalimbali za masomo.  Na nakala hizo ziwiane na maelezo aliyoyatoa katika maelezo binafsi (CV)

Mwombaji anatakiwa kuweka picha ndogo ya “passport size” katika maombi yake.

Umri wa juu uliopo Kisheria ambao unamwezesha mwombaji kuajiriwa katika utumishi wa umma kwa masharti ya kudumu isizidi miaka 45. Ukomo wa umri umewekwa kisheria ili kumwezesha Mwombaji kuchangia mafao yake ya uzeeni kwa miaka 15, maana miaka 15 ndiyo kigezo cha kutimiza masharti ya kulipwa pensheni.  Aidha, kwa wale wenye umri wa zaidi ya miaka 45 wanaweza kuajiriwa kwa mkataba. Hata hivyo baadhi ya nafasi za kazi zinazotangazwa huwa na mahitaji yake maalum ya umri na uzoefu wa kazi husika.

Mwombaji anapaswa kujua kuwa endapo atakuwa amestaafu kazi, ameachishwa kazi, amepunguzwa kazi, amefukuzwa kazi, amestaafishwa kazi kwa manufaa ya umma haruhusiwi kuomba kazi Serikalini, mpaka apate kibali cha Mkuu wa Utumishi wa Umma.

Mwombaji anapaswa kujua kuwa endapo atawasilisha taarifa za kugushi atachukuliwa hatua za kisheria.

Mwombaji anapaswa kujua tarehe ya mwisho ya kuwasilisha Tangazo.
Mwombaji wa kazi/ajira anatakiwa kuzingatia masharti ya jumla ya Tangazo kutofanya hivyo kunamnyima fursa ya kufikiriwa kuajiriwa Serikalini.

Uundaji wa Jopo la Usaili huzingatia aina za waombaji na kada ya nafasi husika kama ifuatavyo;-

Mfano:- Kama nafasi ya kazi ni za Watendaji Wakuu katika Taasisi basi Majopo huwa ni ya Makatibu Wakuu/Wakuu wa Mashirika au Taasisi za Umma.
Kama ni nafasi za Wakuu wa Idara katika Mashirika ya Umma au Taasisi za Umma majopo ya usaili hujumuisha Wakurugenzi au Wakuu wa Idara katika Taasisi za Umma.
Nafasi zilizosalia yaani Kada za chini na nyinginezo basi Majopo yanaundwa na Watumishi Waandamizi.

Kuna tofauti gani katika utaratibu wa ajira unaotumika katika Sekretarieti ya Ajira na ule wa zamani wa kila mwajiri kutangaza na kuajiri? 

Kabla ya Sekretarieti ya Ajira, mwajiri baada ya kupata kibali alikuwa akitangaza nafasi za kazi kwa kuzingatia matakwa ya muundo kwa kila nafasi mpya anayotakiwa kujaza tofauti na ilivyo hivi sasa nafasi za kazi kwa ajili ya ajira huwasilishwa na Mwajiri kwa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira na kumwomba atangaze nafasi hizo pamoja na kufanya mchakato mzima wa kufanya usaili hadi kumpeleka Mtumishi aliyepatikana kwa mwajiri aliyeomba kulingana na mahitaji yake kwa ajili ya hatua za kumwajiri mtumishi husika.

Matangazo ya nafasi za kazi katika Utumishi wa Umma sasa hivi yote yanapaswa kutolewa na Sekretarieti ya Ajira. Hapo awali ilikuwa kila Mwajiri anatangaza, anafanya usaili na kuajiri.

Baada ya kukamilika kwa orodha fupi (shortlisting) Mwajiri alitoa idhini ya kuwaita waombaji wenye sifa katika usaili tofauti na ilivyo hivi sasa baada ya kukamilika kwa orodha hiyo Katibu huitisha kikao cha Wajumbe wa Sekretarieti ya Ajira ambacho huongozwa na Mwenyeketi wa Sekretarieti ya Ajira.  Kikao hiki hupitia orodha hiyo na kisha kutoa idhini ya kuitwa katika usaili.

Baada ya usaili kupitia Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu huandaa taarifa muhtasari wa kikao hicho na kuwasilisha kwa Mwajiri ambako kuna mapendekezo ya Wasailiwa wanaopendekezwa kuajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi.  Tofauti na ilivyo hivi sasa baada ya usaili ni lazima kuandaliwe taarifa ya matokeo hayo na kisha Katibu, huitisha kikao cha Sekretarieti ya Ajira. Kikao hicho hupitia taarifa ya matokeo ya usaili na baadae kutoa idhini ya kuwapangia vituo wasailiwa wote waliofaulu usaili.  Aidha, Sekretarieti ya Ajira hutunza taarifa zote za wasailiwa wote (Data Base) na baadae inapotokea Mwajiri kuhitaji Mtumishi wa aina ambayo tayari imehifadhiwa katika “data base” hupangwa baada ya kuwasiliana na msailiwa pamoja na waajiri.

Ndugu Wahariri na Wanahabari,
Baada ya ufafanuzi huo mfupi, nichukue fursa hii kuwashukuru kwa kunisikiliza.


Ahsanteni sana
Kwa Mawasiliano zaidi;

Katibu,
Ofisi ya Rais,
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
Maktaba Kuu ya Taifa, Ghorofa ya Pili,
Barabara ya Bibi Titi Mohammedi
S. L. P 63100, Dar es Salaam -Tanzania.
Simu; +255 22 2153517
Nukushi; +255 22 2153518
Barua pepe: This e-mail address is being protected from spambots, you need JavaScript enabled to view it
     Tovuti: www.ajira.go.tz

                                                  
 

Visitors Counter

mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday9111
mod_vvisit_counterYesterday19993
mod_vvisit_counterThis week59424
mod_vvisit_counterLast week115954
mod_vvisit_counterThis month59424
mod_vvisit_counterLast month553079
mod_vvisit_counterAll days18714267

Contact Address


Maktaba Complex, Second Floor,
Bibi Titi Mohamed Road
Dar es Salaam
P.O Box: 63100
Tel: +255(22) 2153517
Fax: +255(22) 2153518
Email:katibu@ajira.go.tz

Complaints/Malalamiko: malalamiko@ajira.go.tz
You are here  : Home