October 5, 2017


 

Dkt. Laurean Ndumbaro, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi 

wa Umma na Utawala Bora;

Bibi Rose Magreth Lugembe, Mwenyekiti wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma;

Wajumbe wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma;

Bw. Xavier Daudi, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma;

Wakuu wa Taasisi za Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na 

Utawala Bora mliopo hapa;

Menejimenti na Watumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma;

Waandishi wa Habari;

Mabibi na Mabwana;

Habari za asubuhi.

Awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima na afya njema hasa kuweza kukutana leo kwa ajili ya uzinduzi wa Bodi ya tatu (3) ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, tangu kuanzishwa kwa Sekretarieti hii. 

Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira na Wajumbe, Kabla ya kuendelea na hotuba yangu, napenda nichukue nafasi hii kukupongeza wewe binafsi kwa kuteuliwa  na Mheshimiwa Rais  kuwa Mwenyekiti wa kwanza mwanamke wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma. Ni matumaini yangu na sina shaka kwamba maarifa, ujuzi na uzoefu ulionao kama Katibu Mkuu Mstaafu na mwenye uzoefu wa muda mrefu pamoja na nafasi yako ya Makamu Mwenyekiti katika kipindi kilichopita vitaongeza chachu ya kuongoza vizuri Sekretarieti ya Ajira ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa.

Pia napenda kuwapongeza Wajumbe wote kwa kukubali uteuzi wangu na hivyo kuwa Wajumbe wa  Bodi ya  Sekretarieti ya Ajira.  Niwahakikishieni  ya 

kwamba, uteuzi wenu umezingatia weledi, uzoefu, maadili  na umahiri ambao mliuonyesha wakati mkiwa Watumishi wa Umma. Kama mnavyofahamu jukumu kuu la Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma pamoja na majukumu mengine yaliyoainishwa katika Kifungu cha 29 (4) cha Sheria ya Utumishi wa Umma ni kuendesha michakato ya ajira katika Utumishi wa Umma. Nina imani nanyi kwamba mtatekeleza majukumu yenu kwa weledi na umahiri mkubwa ili kukidhi matarajio ya Serikali.

Meshimiwa Mwenyekiti na ndugu Wajumbe wa Bodi; Kama nilivyosema awali, Bodi yenu ni ya tatu (3) tangu chombo hiki kilipoanzishwa mwaka 2009.  Nitakuwa mchoyo wa fadhila, endapo sitawapongeza 

na kuwashukuru Wajumbe wa Bodi iliyopita. Ninafahamu Wajumbe waliowatangulia walifanya kazi nzuri na kubwa ya kuanzisha taasisi hii na kuijengea 

misingi bora pamoja na taswira nzuri iliyopo sasa. Nawashukuru na kuwapongeza sana. Kwa kuwa taasisi hii imewekewa misingi mizuri na waasisi hao, ndugu Wajumbe  mlioteuliwa sasa pamoja na ubunifu  mnaokuja nao  lakini pia msisite 

kuiga yale mazuri yaliyofanywa na Bodi iliyowatangulia tutapiga hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe wa Bodi; Bodi yenu imeundwa na Wajumbe wenye uzoefu mkubwa katika  masuala ya Utumishi wa Umma, kundi lenu limeundwa na mliokuwa Makatibu Wakuu wa Wizara, Watendaji Wakuu wa Taasisi pamoja na Watumishi Waandamizi kwenye ngazi ya Ukurugenzi. Uzoefu wenu unahitajika sana sio kwa Sekretarieti ya Ajira tu bali kwenye Utumishi wa Umma kwa ujumla. Nasema hivyo kwa sababu, Bodi 

yenu inaanza utekelezaji wa majukumu yake, mwaka mmoja tu baada ya Serikali kuanza utekelezaji wa Mpango  wake  wa Taifa wa miaka mitano wa maendeleo ambao unaishia 2021/22.  Tekelezeni majukumu yenu kwa ufanisi ili muweze kuiwezesha Serikali kufikia malengo ya Mpango wake.

Aidha,  mmeteuliwa katika    kipindi cha miaka michache kabla  ya Taifa letu kufikia mwaka 2025  ambapo tunalenga kuingia  kwenye uchumi wa kati na uchumi wa Viwanda. Kwa hiyo  mnalo  jukumu kubwa la kulipatia Taifa rasilimaliwatu yenye uwezo wa kutuwezesha kutimiza malengo ya Taifa.

Mheshimiwa  Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi; Ajira katika Utumishi wa Umma ni suala  nyeti na la msingi  hivyo ni    muhimu mkasimamia vizuri. Mkifanya kazi ya usimamizi vizuri   Taifa letu litapata nguvu kazi yenye sifa stahiki, weledi na haiba stahiki.  Aidha, endapo taasisi yenu itatoa wasailiwa bora, wenye kukidhi mahitaji ya Waajiri  ninaamini  mtasaidia sana kulifikisha Taifa  letu kufikia malengo  yake inayojiwekea. Hivyo  niwatahadharishe ya kwamba,  eneo hilo lisiposimamiwa kwa  umakini mkubwa linaweza kusababisha Taifa kukosa rasilimaliwatu yenye weledi na  inaweza  kuchangia kuchelewa kufikia malengo yake iliyojiwekea.  Kitu mbacho Serikali ya Awamu ya Tano  haitapenda kitokee.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi; Ili kutekeleza kwa vitendo falsafa ya  HAPA KAZI TU,  Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga utamaduni wa watu kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake  kufanya kazi kwa bidii, weledi na kwa kuzingatia maadili. Hivyo ni wajibu wa Wajumbe wa  Bodi ya  Sekretarieti ya Ajira kushiriki kikamilifu katika kufanikisha azma hii  kwa kuisaidia Serikali kupata Watumishi waadilifu na wenye mwelekeo huo na watakaoweza kwenda na kasi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti; Chombo chenu kimebeba dhamana kubwa sana kwenye uendeshaji wa Nchi yetu. Kama Serikali tunazungumzia mipango mingi na mikubwa, mpango hiyo yote itabebwa na Watumishi wanaoandaliwa na Sekretarieti ya Ajira. Natoa rai kwamba,kwa kushirikiana na Watendaji Taasisi yenu muendelee kuwa wabunifu na kutumia mbinu za kisasa katika utekelezaji  wa majukumu yenu ili rasilimaliwatu mnayoiandaa ikidhi matarajio ya wadau wenu pamoja na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa  Mwenyekiti; Nchi yetu ni kubwa na  Taasisi yenu ni miongoni mwa Taasisi zenye wadau wengi  hasa waombaji wa fursa za ajira  ambao wamesambaa  kwenye kila kona ya Nchi yetu. Andaeni utaratibu ukiwemo wa matumizi  ya Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA) ili muwafikie wadau wenu kwa urahisi zaidi ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia gharama za kuja kufanya usaili Makao Makuu. Pale bajeti inaporuhusu wafuateni wateja wenu na mkaendeshe usaili huko Mikoani.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi; Serikali ya Awamu ya Tano ina matumaini makubwa  sana  kutoka kwenu, nawataka muendelee kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu za ajira, inafahamu muda si mrefu mtaanza kupambana na changamoto za ndugu, jamaa na marafiki ambao wanaamini kuwa uwepo wenu katika chombo hiki  wao  unaweza kuwanufaisha na  wakasaidiwa kiurahisi. Wadau hao waendelee kuelimishwa namna ambavyo wanapaswa kuzingatia matakwa ya Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu za ajira ambapo muombaji yoyote wa ajira Serikalini anapaswa kuwa na sifa stahiki ili aweze kushindania nafasi yoyote wazi inayojitokeza Serikalini. Endapo dhana hii mtaieneza kwa vitendo  ninaamini  itakuwa ni nadra kusikia malalamiko ya upendeleo wa aina yoyote ile.  Katika utekelezaji wa majukumu yenu kama  wasimamizi  wa chombo hiki muhimu, tendeni haki,  upendeleo ama  ubaguzi wa namna yoyote iwe ni mwiko kwenu.  Serikali ina imani nanyi na ndio maana mkapewa kutekeleza jukumu hili, Ninaamini hamtatuangusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi;Suala la ufanisi katika uendeshaji wa michakato ya ajira katika Nchi yetu limekuwa likikabiliwa na changamoto nyingi. Mathalani siku za karibuni tumeshuhudia uwepo wa kiwango kikubwa cha wahitimu wanaotafuta ajira Serikalini. Kutokana  na hali hiyo na ufinyu wa nafasi za ajira Serikalini, yamekuwepo malalamiko na manung’uniko ya namna michakato ya ajira inavyoendeshwa ambayo huenda inachangiwa na waombaji au watendaji wenyewe au mifumo iliyopo ambayo huenda ina mapungufu. Hivyo basi, niwatake mnapoingia kazini pamoja na mambo mengine angalieni mapungufu yanayojitokeza kwenye michakato ya usaili na ajira kwa ujumla na kuja na njia bora zaidi zitakazoleta tija na kuondoa malalamiko yaliyopo. 

Mheshimiwa Mwenyekiti;Kabla sijazindua Bodi ya Tatu ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, nimeombwa nizindue Mkataba wa Huduma kwa Mteja wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ambao ulikwishaanza kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti;Nafahamu kuwa lengo kuu la Mkataba wa Huduma kwa Mteja ni kuwezesha wateja wetu kufahamu majukumu, huduma zinazotolewa na viwango vya utoaji wa huduma hizo kwa kuzingatia taratibu zilizopo. Napenda kutoa rai kuwa, zingatieni Mkataba wa Huduma kwa Mteja pale mnapohudumia wateja na kushughulikia kero za Wananchi. Ni matumaini yangu kuwa mtasimamia na kuhakikisha kwamba ahadi na viwango vya kiutendaji vilivyoainishwa katika Mkataba huo ikiwemo uzingatiaji wa maadili katika utekelezaji wa kazi vinazingatiwa ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti; Baada ya kusema maneno haya machache, sasa natumia fursa hii kutangaza kwamba  Nimeuzindua Rasmi  Mkataba  wa Huduma  kwa Wateja  wa Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wageni Waalikwa na Wanahabari; Baada ya jukumu hilo sasa, napenda kuwatambulisha kwenu Wajumbe wa Bodi ya Tatu ya Sekteratieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma  kama ifuatavyo:-Mheshimiwa  Mwenyekiti  wa  Bodi ya  Sekretarieti ya Ajira  Katika Utumishi wa Umma ni:

Bibi Rose Magreth Lugembe

Wajumbe ni:

(i)  Bw. John Nchwali Joel – Mkurugenzi wa shuguli za Bunge na baadaye Naibu 

Katibu wa Bunge (Mstaafu); 

(ii)  Bw. Mbarak Mohammed ABDULWAKIL  –  Mwalimu na baadaye Katibu Mkuu katika Wizara Mbalimbali (Mstaafu);

(iii)  Bw. Aloyce Lameck Msigwa  –  Katibu Tawala wa Wilaya na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu (Mstaafu);

(iv)  Bw. Fanuel Eusebius Mbonde – Mchumi na Katibu Mkuu (Mstaafu);na

(v)  Bibi Tamika Lutengano Mwakahesya  -  Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Mishahara (Mstaafu).

Mheshimiwa Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi; Baada ya kuwatambulisha, sasa nitumie fursa hii kuwakabidhi vitendea kazi vitakavyowawezesha kutekeleza majukumu yenu kama Wajumbe wa Bodi wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma ambavyo ni:-i.  Marekebisho ya Sheria ya  Utumishi wa Umma  Namba 18  ya Mwaka 2007, ambayo ndiyo yaliyoanzisha Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma;

ii.  Taratibu za Uendeshaji wa Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma za 

Mwaka 2006

iii.  Mpango Mkakati wa  Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi  wa Umma kwa 

Kipindi cha Miaka Mitano (2016/2017 hadi 2020/2021) ; na

iv.  Mkataba wa Huduma kwa Mteja  wa Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa 

Umma wa Mwaka 2017.

Mheshimiwa  Mwenyekiti, Wajumbe wa Bodi, Wageni Waalikwa na 

Wanahabari;

Baada ya hatua hii sasa ninayo heshima kutamka kwamba, 

Nimeizindua Rasmi Bodi ya Tatu ya Sekretarieti ya Ajira Katika

Utumishi wa Umma.

Ninawatakia kazi njema, mafanikio  na Utendaji uliotukuka.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA.