Advertised Posts

Visitors Counter

»Today   473               
»Week   3029               
»Month   20385               
==============
»Total  23338505        

Taasisi za Umma zatakiwa kusimamia Maadili na Utawala Bora.

December 13, 2016


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amezitaka Taasisi zinazosimamia Maadili na Utawala Bora kujisafisha zenyewe kabla ya kuanza kusimamia wengine ili kuepuka kunyooshewa  vidole  katika utendaji kazi wao.

Akizungumza  katika Maadhimisho ya Siku ya Maadili Kitaifa na Haki za Binadamu yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam Mhe. Samia Suluhu amesema kuwa Taasisi zenye jukumu la kusimamia maadili, haki za Binadamu na Utawala bora zinapaswa kujisafisha ili kuwa mfano kwa taasisi nyingine.

“Ni vyema kila Taasisi na wahusika wenye jukumu la kusimamia Maadili, Haki za Binadamu na Utawala Bora kusafisha kwanza nyumba zenu kabla ya kuendelea kusafisha za wengine ili mtakapoenda kuwanyooshea vidole wale nao wasiwanyooshe vidole ninyi” alisisitiza Samia.

Makamu wa Rais aliongeza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa Taasisi zinazosimamia misingi ya Utawala Bora nchini hivyo itaendelea kuziwezesha  Taasisi hizo kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo  kuziwezesha kuendelea  na utoaji haki, kufuatilia majukumu yake kwa mujibu wa  taratibu za  shughuli za Serikali.

Aidha alizitaka Sekta zote za Umma kutekeleza mikataba ya huduma za wateja kama inavyotakiwa kwa kuwa kutofanya hivyo kutakimbiza baadhi ya wawekezaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah Kairuki amesema kwa kuwa suala la maadili na haki za  binadamu ni vitu vinavyoshabihiana,  ameitaka TAKUKURU kuwa na mahusiano na mashirikiano mazuri kati yake na Taasisi nyingine ili kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Kauli mbiu katika maadhimisho hayo ilikuwa kujenga na kukuza maadili, Haki za Binadamu, Uwajibikaji, Utawala Bora na Mapambano dhidi ya Rushwa.