Wajumbe wa Bodi ya zabuni wapewa semina ya mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi wa Umma.

August 19, 2016


Wajumbe wa Bodi ya zabuni na Menejimenti ya Sekretarieti ya Ajira wamepata mafunzo kuhusiana na mabadiliko ya sheria ya ununuzi wa Umma namba 5 ya mwaka 2016 ili kuwajengea uwezo wa kuendana na mabadiliko hayo katika ununuzi wa Umma.

Akifungua Semina hiyo Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amewataka wajumbe wa bodi ya zabuni na Menejimenti hiyo kuyazingatia na kuyatumia mafunzo hayo ili kuweza kuwajengea uwezo wa kiuntendaji unaoendana na mabadiliko ya sheria za ununuzi wa umma na kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria na taratibu katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Ni imani yangu kwamba mafunzo kuhusu mabadiliko ya sheria ya ununuzi wa umma yatawajengea uwezo katika utendaji kazi wenu na kuhakikisha kuwa tunaendelea kufuata sheria, kanuni na taratibu za manunuzi ili kuweza kutoa huduma bora” alisisitiza Daudi.

Kwa upande wake mwezeshaji wa semina hiyo ambaye ni Kaimu mkuu wa kitengo cha huduma za sheria wa sekretarieti ya Ajira Bi. Toni Mbilinyi amesema kuwa semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi ya ununuzi ili kuwaongezea ufanisi katika ununuzi wa umma na kuuwezesha umma kupata thamani ya huduma inayoendana na fedha inayotolewa. Ameongeza kuwa mabadiliko ya sheria ya ununuzi kwa wajumbe itawasaidia kupata uelewa utakawaosadia  katika utekelezaji wa jukumu la ununuzi wa umma kwa manufaa ya nchi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma, 18 Agosti, 2016.