Visitors Counter

»Today   230               
»Week   230               
»Month   16782               
==============
»Total  23367168        

Maswali na Majibu ya Wadau

May 17, 2018


Utangulizi

Tunapenda kukushuru sana wewe mdau wetu ambae umekuwa chachu kubwa ya mabadiliko ambayo tumekuwa tukiyafanya mara kwa mara ili kuhakikisha wadau wetu mnapata huduma inayostahili. Tunakuomba, uendelee kutoa maoni pale unapoona kuna jambo ungependa kupata ufafanuzi au liboreshwe kuhusiana na uendeshaji wa mchakato wa Ajira serikalini tafadhali usisite kuwasiliana nasi ili kupata taarifa sahihi na kwa wakati. Karibu tuijenge nchi yetu kwakuwa na Watumishi wa Umma wenye Sifa, Weledi na Maadili mema.

Ningependa kujua Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilianzishwa kwa Sheria ipi na kwa nini?

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilianzishwa mwezi Machi, 2009 kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu 29 (1). Aidha, katika Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998 toleo Na. 2 la mwaka 2008 Kifungu Na. 4.6 na 6.6.  vimetamka wazi kuwa kitaundwa chombo maalum huru cha kushughulikia mchakato wa masuala ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa niaba ya Wizara, Idara Zinazojitegemea,  Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi mbalimbali za Umma.

Aidha Sekretarieti ya Ajira ilianza kutekeleza majukumu yake ya kuendesha michakato ya ajira rasmi Juni, 2010.  

Lengo mahsusi la kuundwa kwa chombo hiki ni kuziwezesha Mamlaka za Ajira katika ya Utumishi wa Umma kupata nafasi ya kutekeleza majukumu ya msingi kama yalivyoainishwa katika Hati Rasmi (Instruments) zilizoanzisha Taasisi hizo.

Ningependa kufahamu Majukumu ya Sekretarieti ya Ajira ni yapi?

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma mbali na kutekeleza jukumu kuu la kuendesha mchakato wa ajira pia ina majukumu yafuatayo ya kutekeleza kwa mujibu wa Sheria:-

Moja Kutafuta Wataalam wenye ujuzi maalum na kuandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa (kanzidata) za wataalam hao ili kurahisisha utaratibu wa kuwaajiri pindi wanapohitajika;

Mbili Kuandaa orodha ya wahitimu wa Vyuo Vikuu na Wataalam Weledi (Professionals) kwa madhumuni ya kurahisisha rejea na ujazaji wa nafasi wazi za ajira katika Utumishi wa Umma;

Tatu Kutangaza nafasi wazi za kazi zinazotokea katika Utumishi wa Umma;

Nne Kuhusisha wataalam maalum (Appropriate experts) kwa ajili ya kufanya usaili kulingana na mahitaji;

Tano Kutoa ushauri kwa Waajiri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na ajira; na

Sita Kufanya kazi nyingine yoyote inayoendana na majukumu yake kadri itakavyoelekezwa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma

 

Ningependa kufahamu kwa kifupi namna mchakato wa ajira unavyofanyika kupitia chombo hiki kuanzia mnapopokea kibali cha Ajira kutoka kwa Waajiri?

Mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma una historia ndefu na umekuwa ukibadilika kutegemeana na mahitaji ya wakati tangu wakati wa uhuru hadi sasa.

Kwa kuwa Sekretarieti ya Ajira imekabidhiwa dhamana ya kuendesha mchakato wa Ajira kwa niaba ya Waajiri ndani ya Utumishi wa Umma, imekuwa ikitekeleza jukumu hilo kwa utaratibu ufuatao;-

Kwa hatua za awali, Sekretarieti ya Ajira hupokea vibali vya Ajira kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi kwa ajili ya kuendesha mchakato wa Ajira kwa niaba ya Waajiri ili kujaza nafasi mbalimbali zilizo wazi. Vibali hivyo vinaweza kuwa vya aina mbili:-

 Vibali vya Ajira Mpya – Vibali hivi hupatikana kutokana na Ikama ya kila mwaka wa fedha kulingana na mahitaji ya Taasisi husika ama

Vibali vya Ajira Mbadala – vibali hivi hupatikana baada ya kutokea upungufu wa mtumishi/watumishi katika Taasisi, aidha kwa kufariki, kuacha kazi, kuachishwa kazi, kustaafishwa kazi kwa manufaa ya Umma au kustaafu.

Hatua ya pili, Sekretarieti ya Ajira baada ya kutambua nafasi zinazohitajika kujazwa kwa mujibu wa vibali vilivyowasilishwa upitia Miundo ya Utumishi ya kada husika kwa kuainisha sifa zinazohitajika na kwa kushirikiana na Waajiri husika huandaa tangazo la kazi, ambalo hutolewa kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Ajira (www.ajira.go.tz). Muda unaotolewa kwa waombaji kazi kuwasilisha maombi yao kwa wale wenye sifa zilizoainishwa ni siku 14 tokea tokea tarehe ya tangazo kutolewa kwa mara ya kwanza.

Hatua ya tatu, Baada ya muda uliopangwa wa kupokea maombi kupita yaani siku 14 zilizotajwa hapo juu, Sekretarieti ya Ajira uandaa orodha ndefu ya waombaji wote waliowasilisha maombi na hatua inayofuata ni kufanya uchambuzi wa orodha hiyo kulingana na sifa zinazohitajika zilizotolewa katika tangazo kupata orodha fupi ya waombaji wenye sifa kwa mujibu wa vigezo wanaopendekezwa kuitwa katika usaili. Zoezi hilo huchukua takribani muda wa siku 7 hadi 14 kulingana na idadi ya waombaji walioomba kazi.

Hatua ya nne, Baada ya orodha fupi kukamilika, Sekretarieti ya Ajira mara kadhaa ukaribisha Waajiri kupitia nao pamoja orodha hiyo ambayo baadaye huwasilishswa kwenye kikao cha Wajumbe wa Sekretarieti ya Ajira kwa ajili ya kuipitia, kujiridhisha na kuidhinisha majina ya waombaji wenye sifa waliopendekezwa ili waweze kuitwa kwenye usaili utakaopangwa kulingana na kada zinazohusika.  

Katika hatua hii ya usaili Sekretarieti huendesha saili za aina tatu kwa sasa kulingana na kada.

Usaili wa Mchujo (Usaili wa kuandika) - Huu hufanyika endapo idadi ya nafasi zinazohitajika kujazwa ni chache na waombaji ni wengi- lengo kupata wale watakaofaulu kuingia katika hatua inayofuata. Usaili huu upima uelewa wa masuala ya jumla, ama wa kitaaluma.

Usaili wa Vitendo (Practicals)- Usaili huu hufanyika kwa kada ambazo kazi zake ni za vitendo zaidi, lengo kuu ni kumpima mwombaji wa kazi kufahamu endapo ana ujuzi wa kile anachotarajiwa kukifanya. Mfano Madereva, Maafisa Tehama, Makatibu Mahsusi, Walinzi, Wahifadhi Wanyamapori na nyinginezo.

Usaili wa Mahojiano (Oral Interview)- Usaili huu ni wa mahojiano ya ana kwa ana ambayo hulenga kumpima mwombaji wa kazi ujuzi wake katika kujieleza, haiba, kujibu maswali ya kitaalam ya kada yake, uzingatiaji wa muda na vigezo vingine.

Hatua ya tano: Baada ya orodha ya waombaji waliopendekezwa kuitwa katika usaili kuidhinishwa Sekretarieti ya Ajira huandaliwa tangazo ambalo pia hutolewa kwenye tovuti kuwaita waombaji kazi walioidhinishwa kuhudhuria usaili kwa tarehe iliyopangwa. Tangazo la kuwaita waombaji kwenye usaili utolewa kwa muda wa muda wa siku 7 na kuendelea kutegemeana na wakati na mahitaji.

Hatua ya sita, Baada ya kutoa tangazo la kuwaita waombaji wenye sifa kwenye usaili Sekretarieti ya Ajira kwa kushirikiana na Waajiri huandaa majopo ya usaili kulingana na kada zinazosailiwa. Washiriki ama Wajumbe wa majopo ni Wataalamu kutoka Taasisi mbalimbali ndani ya Utumishi wa Umma wanaoshirikiana na Watendaji wa Sekretarieti ya Ajira katika zoezi zima la usaili kwa lengo la kupata waombaji kazi wenye sifa na weledi unaotakiwa. 

Hatua ya saba: Baada ya usaili kufanyika matokeo ya usaili huo huwasilishwa katika kikao cha Wajumbe wa Sekretarieti ya Ajira kwa ajili ya kuidhinishwa na kupitishwa ili waombaji waliofaulu waweze kupangiwa vituo vya Kazi.

Hatua ya nane, Baada ya wasailiwa waliofaulu kuidhinishwa hupangiwa vituo vya kazi, na kutaarifiwa kufika kuchukua barua zao za kupangiwa vituo kupitia anuani zao. Mawasiliano juu ya hatua hiyo kwa wasailiwa hufanyika kwa njia ya tangazo linalotolewa kupitia tovuti ya ofisi ya Sekretarieti ya Ajira. Waombaji waliofaulu na kupangiwa vituo vya baada ya kupata barua wanatakiwa kuripoti kituo cha kazi ndani ya siku 14.

Ni vyema ukafahamu kuwa kutokana na hatua hizi mchakato huo mzima kama nilivyofafanua hapo juu huchukua takribani siku hamsini na mbili (52) kwa sasa baada ya kuboresha mfumo wa kupokea maombi kwa njia ya kieletroniki tofauti na hapo awali ilikuwa ikichukua zaidi ya siku 90 hadi kukamilika wakati njia ya posta ilipokuwa ikitumika kupokea maombi ya kazi kutoka kwa waombaji.

Kwakuwa Sekretarieti ya Ajira ndio yenye jukumu la kuendesha mchakato wa Ajira kisheria katika Utumishi wa Umma sasa ningependa kufahamu kwa kifupi namna Mchakato wa Ajira katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa unavyofanyika kwa kushirikiana nanyi?

Ili kukidhi mahitaji ya sasa ya Serikali, Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 ilifanyiwa marekebisho na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira amepewa uwezo wa kukasimu kazi na madaraka yake kwa Afisa Mtendaji Mkuu au kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kuendesha mchakato wa ajira kama ataona inafaa. Taarifa ya kukasimu madaraka hayo ilitolewa kwenye gazeti la Serikali Na.70 la mwaka 2014. Kutokana na marekebisho hayo ya Sheria, Serikali za Mitaa na Vyuo Vikuu vya Umma kumi na moja (11) zimekasimiwa mamlaka ya kuendesha mchakato wa kada za chini 22 na na kada za kitaaluma mara watakapoendesha mchakato huo uwakilishi wa Sekretarieti ya Ajira unapaswa kuwepo ili kuangalia endapo taratibu zimefuatwa na kujiridhisha kuwa anaepata kazi ndiye aliyestahili kwa haki.

Ningependa kufahamu Matumizi ya TEHAMA katika kuendesha mchakato wa Ajira na je yamewaongezea tija yoyote?

Moja; Mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia yameleta mapinduzi makubwa katika maeneo mengi ikiwemo Ajira Serikalini ambapo imeweza kupanua wigo wa mawasiliano na kutoa nafasi kwa kila mtu anaetafuta fursa ya ajira kuweza kupata taarifa ya nafasi ya kazi kwa haraka popote alipo pindi inapotangazwa kupitia njia ya kieletroniki;

Mbili;TEHAMA imerahisisha na kuwawezesha wale wote wanaotafuta kazi kuweza kuomba fursa za kazi bila kujali mahali walipo, wakati wa kutuma maombi, kufahamiana ama kutofahamiana na watumishi wa ofisi yenye ajira ilimradi ni  watanzania wenye sifa stahiki kwa mujibu wa nafasi ya kazi iliyotangazwa;

Tatu; Ili kupunguza gharama za uendeshaji na kutafuta njia rahisi ya kuwafikia wananchi popote walipo kwa sasa Sekretarieti ya Ajira inatangaza nafasi za kazi zilizopo katika Utumishi wa Umma na kupokea maombi yote ya kazi kwa njia ya kielektroniki zaidi kupitia Tovuti yake ya  www.ajira.go.tz na kupitia “Recruitment Portal” (portal.ajira.go.tz);

Nne; Mfumo huu wa upokeaji wa maombi ya kazi kwa njia ya kielektroniki ujulikanao kama Recruitment Portal (portal.ajira.go.tz) ni rahisi kuutumia pindi mtu akishajisajili katika mfumo maana humuwezesha mwombaji kazi kuweka taarifa zake zote za msingi zikiwemo za kitaaluma ambapo anaweza kuzitumia muda wowote kuziboresha kwa kuongeza taarifa au kuondoa taarifa pindi anapohitaji kufanya hivyo.

Tano; Mfumo huu umewasaidia waombaji kazi wengi kupata mahali salama pa kuhifadhi nyaraka zao, umewapunguzia gharama za kutoa nakala kila kazi inapotangazwa kwa kuwa taarifa zikishawekwa mara moja ni mwombaji mwenyewe kuamua kubadiisha kila atakapotaka kuzitumia kulingana na mahitaji yake.

Sita; Mfumo umewasaidia waombaji kazi kutumia muda mfupi sana kuwasilisha maombi huku wakiwa na uhakika wa maombi kufika na kupata mrejesho wa kile alichowasilisha papo hapo kama kimepokelewa.

Ningependa kufahamu Fursa za Walemavu katika Mchakato wa Ajira kwa mujibu wa Sheria zikoje na je mnazingatia hilo?

Sekretarieti ya Ajira inasimamia Sheria, Kanuni na Taratibu katika kutekeleza mchakato wa Ajira Serikalini.

Sheria ya Walemavu Sura 183, Kifungu cha 33 (1) kimeeleza wazi utaratibu unaotakiwa kufuatwa wakati wa kutekeleza mchakato wa Ajira ndani ya Utumishi wa Umma. Sambamba na Sheria hiyo pia Kanuni za Uendeshaji za Sekretarieti ya Ajira za mwaka 2009, Kanuni ya 16 (1) imeainisha wazi wastani anaotakiwa kufikia kila msailiwa ili aweze kuajiriwa kuanzia madaraja ya kuingilia, nafasi za Wanataaluma hadi ngazi ya Watendaji Wakuu.

   Kwa msingi huo Sekretarieti ya Ajira imeweka wazi katika mfumo wake wa uwasilishaji wa maombi ya kazi ikiwataarifu Waombaji wa fursa za Ajira kuainisha katika mfumo na hata kueleza kwenye barua endapo ni mlemavu ili kwanza kuweza kumwandalia mazingira rafiki kulingana na hali yake ili aweze kufanya usaili bila ya matatizo.

    Sambamba, na hilo pindi inapotokea kuna mlemavu aliyefanya usaili na kufikia wastani unaotakiwa na kufungana na wasailiwa wengine basi msailiwa mwenye ulemavu hupewa kipaumbele cha kupata Ajira.

Ningependa kufahamu baadhi ya Mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa?

Kabla ya kujibu swali lako ningependa ufahamu kuwa Sekretarieti ya Ajira inatoa huduma za kuendesha mchakato wa Ajira Serikalini pamoja na kutoa ushauri na utaalamu katika eneo hili. Hivyo, mafanikio yake makubwa ni kuona wadau wake wanapata Watumishi bora na makini, wanapata huduma nzuri na kwa wakati, baada ya maelezo haya sasa niainishe baadhi ya mafanikio ya kuwa na chombo hiki kama ifuatatavyo;-

Moja;  Sekretarieti ya Ajira imeweza kutoa huduma ya kuendesha mchakato wa Ajira kwa niaba ya mamlaka za ajira mbalimbali, kubadilishana uzoefu na mamlaka nyingine za Ajira ndani ya Utumishi wa Umma na sekta binafsi, kuwaelimisha wadau kuhusu uendeshaji wa mchakato wa ajira pamoja na majukumu ya chombo hiki.

Mbili; Sekretarieti ya Ajira imeweza kuendesha zoezi la usaili katika Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar kulingana na hali ya fedha iliporuhusu kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wadau pamoja na kuwapunguzia gharama wasailiwa za kusafiri hadi Dar es Salaam.

Tatu; Sekretarieti ya Ajira imewapangia wasailiwa waliofaulu usaili vituo vya kulingana na mahitaji ya Waajiri kama yalivyoainishwa katika vibali husika vya ajira.

Nne; Sekretarieti ya Ajira kwa kiasi kikubwa imesaidia Serikali kupunguza tatizo la ukosefu wa Watumishi wa kutosha kwa baadhi ya maeneo ambayo awali yalionekana kukosa wataalam hasa maeneo ya pembezoni. Suala hili linaenda sambamba na kuajiri watumishi wenye sifa na kupunguza tatizo la ukabila, rushwa na upendeleo kwa kuhakikisha mchakato wa ajira unazingatia misingi ya haki, usawa na uwazi kwa kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

Tano; Sekretarieti ya Ajira imeweza kuendelea kuboresha mifumo yake ya mawasiliano na utoaji huduma  kwa wadau wake kupitia njia zifuatazo;-

 Tovuti ya Taasisi ambayo ni (www.ajira.go.tz), iliyoanzishwa tarehe 25 Aprili, 2012 ambapo ni takribani miaka sita sasa imeshatembelewa zaidi ya mara 23,302,585 hadi tarehe 17 Mei, 2018.   

 “Recruitment Portal” (portal.ajira.go.tz) ambao ni Mfumo wa uwasilishaji wa maombi ya kazi kwa njia ya kielektroniki

Ili kwenda na kasi na kuwafikia Wahitimu ambao wengi ni vijana ambao ni miongoni mwa wadau wetu wakubwa katika Ajira tumefungua anwani katika mitandao ya kijamii ikiwemo facebook (www.facebook.com/sekretarieti) na mitandao mingine ni pamoja na Instagram (psrsajira), twitter.com/psrsajira na Youtube yote hii ni ili kupanua wigo wa utoaji wa taarifa na mawasiliano na wadau kwa karibu zaidi.

Sambamba na mbinu nilizoainisha hapo juu, Sekretarieti ya Ajira kupitia matumizi ya barua pepe za Vitengo mbalimbali na huduma tofauti iliona kuna umuhimu wa kuwa na barua pepe maalum za kuwawezesha wadau kutuma maoni, kuandika hoja, kuuliza maswali na hata kuwasilisha malalamiko yao na kupatiwa majibu/ufafanuzi miongoni mwa barua pepe hizo ni pamoja na  gcu@ajira.go.tz, malalamiko@ajira.go.tz, tehama@ajira.go.tz, zanzibaroffice@ajira.go.tz

Licha ya kuanzisha njia zote hizo za mawasiliano bado tuliona kuna haja ya kuwa na simu za kiganjani kwa ajili ya wadau kuweza kupiga moja kwa moja na kupata huduma ya papo hapo kupitia namba zifuatazo 0784-398259 Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa tatizo lolote la mifumo ya maombi ya kazi, 0687-624975 Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa uendeshaji wa mchakato wa Ajira hususani majukumu ya Taasisi na matangazo ya nafasi za kazi.

Aidha, Sekretarieti ya Ajira imepunguza hoja na malalamiko ya wadau kwa kiasi kikubwa kwa kutumia mfumo wa utumaji wa ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu za viganjani (Bulk sms). Ijapokuwa lengo la awali la kutumia njia hii ilikuwa ni kurahisisha na kuharakisha utoaji wa taarifa kwa waombaji kazi waliofanikiwa kuitwa katika usaili.

Pamoja na njia hizo zote lakini kutokana na unyeti wa suala la ajira bado Taasisi iliona kuna umuhimu wa kuwa na dawati la Msaada (help desk) wa huduma tunazozitoa katika Sekretarieti ya Ajira kwa ajili ya kujibu hoja na maswali mbalimbali ili kuwawezesha wananchi na wadau mbalimbali wanaofika ofisini kwetu moja kwa moja na kupata huduma ya ushauri n.k.

Vilevile Sekretarieti ya Ajira imefanikiwa kuanzisha, kutumia na kuimarisha usimamizi wa Mfumo wa kuhifadhi taarifa (kanzidata) ya waliofaulu usaili ili kurahisisha utaratibu wa kuwapangia pindi wanapohitajika. Aidha, mfumo huu umekuwa na faida kubwa kwa Serikali, Taasisi na hata wadau wakuu ambao ni (wasailiwa) kutokana na kurahisisha ujazaji wa nafasi, kuokoa muda na gharama kwa wadau na Serikali za kuendesha mchakato wa Ajira mara kwa mara.

Halikadhalika, Sekretarieti ya Ajira kutokana na matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa maombi ya kazi, imefanikiwa kupunguza siku za uendeshaji mchakato wa Ajira kutoka siku 90 hadi siku 52.

Sekretarieti ya Ajira tangu kuanza kutolewa kwa vibali vya ajira baada ya kusitishwa kwa mwaka 2016/17 imefanikiwa kuzuia waombaji kazi waliowasilisha maombi yao ya kazi kupitia Sekretarieti ya Ajira zaidi ya 45, lakini kabla ya hapo tuliponza mwaka 2010 hadi 2015/2016 tulizua waombaji kazi 1951 waliotaka kutumia vyeti na nyaraka za kughushi ili kujipatia fursa ya kuajiriwa katika Utumishi wa Umma bila ya kuwa na sifa stahili.

      Kwakuwa popote kwenye Mafanikio hapakosi Changamoto ningependa kufahamu zile changamoto za jumla mnazokabiliana nazo na namna mnavyozikabili kwa ufupi?

Moja, Baadhi ya wadau kuwa na fikra hasi (mindset) kuhusiana na upendeleo, rushwa n.k. Katika changamoto hii, tunaendelea kuelimisha Umma kuhusu Sekretarieti ya Ajira inavyofanya kazi pamoja na kuhakikisha tunatoa huduma kwa wakati, viwango, uwazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu.

Mbili Sekretarieti ya Ajira imekumbana na uwepo wa baadhi ya waombaji wa kazi kughushi sifa za kielimu, taarifa binafsi, nyaraka na pia sifa za kitaaluma. Changamoto hii tumekabiliana nayo kwanza kwa kuwaondoa katika mchakato wale wanaobainika kufanya hivyo pamoja na kuendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti ndani ya taasisi ili kuhakikisha Serikali inapata watumishi wenye sifa stahiki na si vinginevyo.

Tatu, Vitendo vya ulaghai/utapeli vinavyofanywa na baadhi ya watu kwa kutumia jina la Sekretarieti ya Ajira kuomba fedha kutoka kwa waombaji wa fursa za ajira kwa ahadi ya kuwapatia ajira. Changamoto hii nayo tumekuwa tukiiitolea ufafanuzi na taadhari na tutaendelea kulitilia mkazo pamoja na kuwasilisha taarifa kwa vyombo vya dola ili kuweza kukabiliana nalo na kuwaepusha wadu wetu kutokukubali kurubuniwa na matapeli hao na kupata hasara.

Nne; Baadhi ya Wahitimu kuwa na uwezo mdogo; Asilimia kubwa ya wasailiwa kuwa na  uwezo mdogo wa kujieleza kwa lugha rasmi za usaili ambazo ni Kiswahili na Kiingereza na hivyo kushindwa kuwasilisha vizuri majibu ya usaili kwa kile alichofundishwa chuoni na hivyo kupelekea Sekretarieti ya Ajira wakati mwingine kushindwa kujaza baadhi ya nafasi na kurudia upya mchakato mzima. Changamoto hii nayo tumeendelea kutoa mrejesho kwa wahusika ikiwemo wahitimu na waalimu pamoja na kuwasaidia wale walioko vyuoni kwa kuwatembelea wakiwa huko na kuomba fursa ya kuzungumza nao na kuwaonyesha changamoto zilizopo na nini kifanyike kwa yale ambayo tunauwezo wa kurekebisha yamekuwa yakifanyika hivyo.

Tano;Baadhi ya Mifumo ya kieletroniki ya taarifa na huduma ndani ya Serikali na taasisi nyingine zisizo za kiserikali kutozungumza kwa pamoja; Mifumo mingi ya taarifa ndani ya Serikali mfano mifumo ya Taasisi zikiwemo TCU, NECTA, NIDA, RITA, n.k haizungumzi pamoja hivyo kupelekea Sekretarieti ya Ajira kupata ugumu wa kuhakiki taarifa za wasailiwa wanazoziwasilisha katika kuendesha mchakato wa ajira ili kuwapata waombaji wenye sifa. Ili kufanikisha dhamira hiyo tupo kwenye mchakato na baadhi ya mifumo imeanza kuhuishwa kwa pamoja kazi hiyo itakapokamilika taarifa za waombaji kazi zitaweza kupatikana kwa haraka baadhi ya Taasisi hizo ni pamoja na TCU, NECTA, NACTE, NIDA, RITA, na taasisi nyingine.

Sita;Uelewa mdogo wa Wadau kuhusu Majukumu ya Sekretarieti ya Ajira. Ofisi imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa Umma  kwa kuandaa vipindi vya redio na runinga pamoja na kutumia fursa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, mikutano, usaili na maonesho mbalimbali ili kuendelea ikiwa ni pamoja na kuanzisha dawati/simu za kiganjani kwa ajili ya kujibu hoja/maswali mbalimbali ya wadau papo hapo ili kukuza uelewa na kuboresha utoaji wa huduma.

Saba,Mbali na changamoto zilizoainishwa katika swali namba nane. Ningependa kufahamu ni vitu gani mwombaji kazi asipotekeleza anaweza kukosa nafasi ya kuitwa kwenye usaili hata kama atakuwa anasifa za kuajiriwa katika nafasi husika?

 1. Waombaji kazi wengi kutokufahamu namna ya kuandika barua za maombi ya kazi; mfano mwombaji kuandika maombi ya kazi tofauti na iliyotangazwa;
 2. Waombaji kazi kutokusaini barua za maombi ya kazi (barua zinapaswa kusainiwa, kunakiriwa (scan) na kushikizwa (attach)katika mfumo;
 3. Waombaji kazi kutokuthibitisha nyaraka zao (certify) katika mamlaka husika;
 4. Waombaji wengi kutozingatia vigezo vya nafasi iliyotangazwa, ikiwemo kudanganya sifa wakidai wamemaliza shahada ya fani fulani ilihali hawajasoma shahada ya aina hiyo, au mwombaji mwenye elimu ya astashahada kuomba kazi ya shahada;
 5. Waombaji kazi kutokuambatisha nyaraka za elimu hususani ACSE, CSE, au astashahada, stashahada na shahada walizosoma;
 6. Waombaji kazi ambao ni Waajiriwa katika Utumishi wa Umma kutokupitisha barua za maombi yao kwa Waajiri wao kabla ya kuziwasilisha Sekretarieti ya Ajira; (Kupitisha barua kwa Mwajiri inasaidia kuthibitisha kuwa endapo msailiwa atapata nafasi anayoomba Mwajiri atakuwa tayari kumruhusu kutoka kujaza nafasi aliyoomba).
 7. Waombaji kazi waliosoma nje ya nchi kutowasilisha vyeti vyao vya uthibitisho wa kutambulika elimu walizozipata nje ya nchi katika mamlaka husika kama NECTA, NACTE na TCU kabla ya kuzituma Sekretarieti ya Ajira;
 8. Waombaji kazi wengi kuandika wadhamini ambao ni ndugu zao badala ya wadhamini wanaoweza kutoa taarifa zao za kitaaluma na kikazi kwa uhuru;
 9. Waombaji kazi kuandika barua moja ya kuombea kazi kwa nafasi tofauti;
 10. Waombaji kuandika wasifu binafsi bila ya kuweka taarifa zao muhimu (jina, elimu yake, namba za mawasiliano, kozi alizohudhuria nk.na badala yake kuandika masuala yasiyo na umuhimu sana kama vile (masuala anayopendelea hobbies nk. (CV);
 11. Baadhi ya waombaji kazi kupakia katika mfumo picha zisizohitajika badala ya Pasportsize mfano aina ya picha  zinazopigwa, maeneo yanayotumika kupigia picha hizo pamoja na mavazi yanayovaliwa;
 12. Baadhi ya waombaji kazi kuja kwenye usaili wa mchujo au mahojiano bila ya vyeti vyao halisi kama inavyoelekezwa;
 13. Waombaji kazi wengi kutozingatia masharti ya jumla ikiwemo:
 1. Kuwasilisha maombi, kwa njia tofauti na ile iliyoelekezwa kwenye tangazo la kazi,
 2. kuwasilisha taarifa za uongo mfano, wasifu binafsi usio wa ukweli,
 3. kutopakia taarifa sahihi (upload) katika maeneo husika ya mfumo wa maombi ya kazi,
 4. Kupakia vyeti visivyokamilika mfano result slips, partial transcript, provisional result, progress report, statement of result nk.
 5. Baadhi ya Walemavu kutojulisha Mamlaka hali zao.

Sekretarieti ya Ajira inatoa rai/mwito kwa wadau wetu kama ifuatavyo;

Wito kwa Waajiri;Kwa upande wa Waajiri Waliokasimiwa jukumu la kuendesha mchakato wa Ajira nchini  wanakumbushwa umuhimu wa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu pamoja na uwazi katika kutekeleza kazi hii ili kuiwezesha Serikali kupata watumishi wenye weledi, sifa na uwezo  wa kufanya kazi ili kuweza kuleta maendeleo katika Taifa letu kwa ujumla.

Ushauri kwa waombaji kazi;

Kwanza; Wawe na utaratibu wa kuweka kumbukumbu za matangazo au kazi wanazoomba ili kuwa na rejea ya baadae.

Pili; Wajiwekee utaratibu wa kufungua tovuti ya Sekretarieti ya Ajira www.ajira.go.tz angalau mara moja kwa kila wiki ili waweze kupata taarifa mbalimbali ikiwemo fursa za ajira zilizopo ama hatua mbalimbali za mchakato wa Ajira kwa nafasi zilizoshatangazwa.

Tatu;Kujisajili kwenye mfumo mapema na kupakia taarifa sahihi na pale wanapokuwa na changamoto kuwasiliana na Sekretarieti ya Ajira moja kwa moja au kuja ofisini kabla ya tangazo la kazi kufungwa ili kupata msaada.

Nne, Kuzingatia masharti na vigezo vinavyowekwa kwenye tangazo kabla ya kuwasilisha maombi yao ya kazi.

Tano; Kujiandaa vyema kwa ajili ya usaili ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata kazi wanazoziomba.

Sita; Kuuliza maswali moja kwa moja kwa Taasisi kupitia njia za mawasiliano zilizoainishwa katika baadhi ya majibu ya maswali haya ili kuweza kupata majibu sahihi na kwa wakati jambo ambapo litasaidia kuepuka kupata taarifa za kupotoshwa katika baadhi ya mifumo mingine ya mawasiliano wanayotumia.

 Karibu tuijenge nchi yetu kwakuwa na Watumishi wa Umma wenye Sifa, Weledi na Maadili mema.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI, SEKRETARIETI YA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA. Tarehe 17 Mei, 2018.