Visitors Counter

»Today   224               
»Week   224               
»Month   16776               
==============
»Total  23367162        

Sekretarieti ya Ajira yatoa elimu ya masuala ya Ajira Serikalini kwa Wanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Mtwara.

December 11, 2017


Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imefanya ziara ya kikazi katika Chuo  Chuo cha Utumishi wa Umma tawi la Mtwara ikiwa ni hatua endelevu ya utekelezaji wa mkakati wake wa kutatua changamoto  mbalimbali ambazo zimekuwa zikibainika wakati wa utekelezaji wa mchakato wa Ajira Serikalini kwa kukutana na wadau wake ikiwemo wanafunzi wa vyuo mbalimbali Nchini.

Katika ziara hiyo mada mbalimbali  zilitolewa  kwa Wanafunzi wa Chuo hicho ikiwemo taratibu za uendeshaji wa  Mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma, Masharti ya msingi ya kuzingatiwa kabla na baada ya kuwasilisha maombi ya kazi, Matumizi ya TEHAMA hususani maelekezo ya kujisajili katika mfumo wa maombi ya kazi (Recruitment Portal).

Afisa Mawasiliano kutoka, Sekretarieti ya Ajira ktika Utumishi wa Umma Bw. Kassim Nyaki akiongea na wanafunzi wa chuo hicho alibainisha kuwa mada hizo zimelenga kutatua changamoto pamoja na kutoa uelewa kwa wanafunzi wa Vyuo ili watakapohitimu waweze kujua majukumu ya Sekretarieti ya Ajira, taratibu za kufuata kabla ya kuomba ajira Serikalini, namna ya kujiandaa kabla na wakati wa usaili pamoja na utaratibu wa uwasilishaji wa maombi ya kazi kwa njia ya mtandao ujulikanao kama Recruitment portal.

 

“Sekretarieti ya Ajira tunatambua kuwa nyie ni kati ya wadau wetu wakubwa katika kutekeleza Mchakato wa Ajira Serikalini, na tunatambua baada ya kuhitimu masomo wengi wenu mmejipanga kuingia katika soko la ajira  ambalo linahitaji watu wenye maadili, weledi na uelewa wa kutosha katika masuala mbalimbali” alisisitiza Nyaki.

Nyaki aliongeza kuwa, Sekretarieti ya Ajira katika kukabiliana  na changamoto inazokumbana nazo wakati wa uendeshaji wa mchakato wa Ajira imeamua kuwa na mkakati wa kuwafuata wadau wake kuzungumza ili kuwaelimisha  na kupata mrejesho kutoka kwao ili wanapoanza kuwasilisha maombi ya kazi kupitia Sekretarieti ya Ajira tayari wawe na uelewa na kufahamu vyema taratibu za kuomba kazi, namna ya kuandaa wasifu binafsi (CV) namna ya kuandika  barua za maombi ya kazi, jinsi ya kujiandaa kabla na wakati wa usaili na utaratibu mpya wa utumaji na upokeaji wa maombi ya kazi kwa njia ya Mtandao ujulikanao kama Recruitment portal”  ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuweza kushindana katika soko la ajira nchini.

Katika ziara hiyo Afisa TEHAMA kitoka Sekretarieti ya Ajira Bw. Musa Mselem alitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa vitendo (Practical) ya namna ya kujiunga katika Mfumo wa maambi ya kazi kupitia ‘Portal’ ya ajira.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Utumishi wa Umma Dr. Henry Mambo amewashauri wanafunzi wa Chuo hicho kutambua kwamba soko la Ajira lina ushindani mkubwa kwa kuwa wahitimu ni wengi hivyo ni lazima wajiandae kisaikolojia kushindana katika soko hilo na kupata fursa ya kuajiriwa Serikalini.

Ziara hiyo ni muendelezo wa mkakati Sekretarieti ya Ajira kutembelea wadau wake ikiwemo Waajiri na Wanafunzi wa Vyuo mbalimbali nchini ili kuweza kuwajengea uwezo katika maeneo ambayo imekuwa ikibaini mapungufu badala ya kuendelea kubaki maofisini.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.